Mameneja rasilimali watu ‘tiba’ afya ya akili kwa watumishi
KWA miaka ya karibuni kumekuwa na wimbi la watu wanaojidhuru kwa kujitoa uhai kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kimapenzi na ugumu wa maisha.
Matukio hayo yamekuwa yakihusisha vifo vya kujiua ama mwanaume au mwanamke kuua mwenzi wake na wakati mwingine mzazi kuua watoto wake.
Mara kadhaa sababu za kufanya hivyo imeelezwa ni wivu wa kimapenzi, ugumu wa maisha na msongo wa mawazo.
Mhusika huona hana suluhisho zaidi ya kujiua/kuua ama kuingia kwenye ulevi kupindukia akiamini ndio suluhisho la tatizo linalomkabili.
Wataalamu wa magonjwa ya akili wanasema hatua ya mtu kujidhuru au kumdhuru mwenzake kwa sababu yoyote ile, hutokana na tatizo la afya ya akili.
Afya ya akili ni tatizo linalomfanya mtu kuwa na hisia na hatua ya kufanya matendo tofauti yasiyotarajiwa kwenye jamii.
Ndio maana mtu anaweza kunywa sumu, kujinyonga, kuwa mlevi kupindukia hiyo husababishwa na hisia zinazotokana na tatizo la afya ya akili.
Asilimia kubwa kwa sasa ya wanaopatwa na tatizo la afya ya akili ni vijana na ikiwa hawatachukua hatua, huendelea kuteseka mpaka wanapokuwa watu wazima.
Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika nchini mwaka jana (2022) na kuonesha Tanzania ina idadi ya watu 61,741,120, asilimia zaidi ya 40 ni vijana.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema matatizo ya afya ya akili mara nyingi husababisha msongo wa mawazo, kujiua, unywaji pombe kupita kiasi na matumizi ya mihadarati.
Hayo yote husababisha vifo kwani ulevi kupindukia hufanya wakati mwingine mtu kuendesha gari hovyo na kupata ajali, lakini pia ulevi husababisha kufanya ngono isiyo salama hali inayoweza kuleta magonjwa ya kuambukiza na baadaye vifo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres anashauri serikali kuona umuhimu wa kuwekeza katika afya, elimu na jamii katika kudhibiti janga hilo ili kuhakikisha ajenda ya mwaka 2030 ya maendeleo haimuachi mtu nyuma ikiwemo vijana wenye matatizo ya afya ya akili ambao wakati mwingine hunyanyapaliwa na kukosa msaada kutokana na hali yao.
Ikiwa wataalamu wanasema kundi la vijana na watu wazima ndio waathirika wakubwa, basi hali si salama katika maeneo ya ofisi mbalimbali na hii ni hatari pia kwa familia, jamii na nchi nzima.
Sekta ya meneja rasilimali watu ni muhimu sehemu za kazi, kwani mtu huyu ni kiunganishi kati ya wafanyakazi na uongozi.
Karibu matukio mengi kwenye maofisi huwahusisha watu hawa kwa namna moja ama nyingine, jambo linalowalazimu kuwa karibu na wafanyakazi.
Msongo wa mawazo, unywaji pombe kupindukia ni moja ya masuala yanayomhusu meneja rasilimali watu moja kwa moja endapo mmoja wa wafanyakazi wa taasisi yake atakuwa na tatizo hilo, ili kunusuru nguvu kazi ya kampuni.
Katika kuhakikisha tatizo hilo la afya ya akili linamalizwa, kwenye mkutano mkuu wa Jumuiya ya Afrika katika masuala ya Utawala na Uongozi, (AAPAM Chapter Tanzania), mameneja rasilimali watu pamoja na mambo mengine, walipewa somo kuhusu tatizo la afya ya akili.
Mkutano huo ulifanyika Aprili 27 kwenye ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam na kuhudhuriwa na mameneja rasilimali watu kutoka taasisi mbalimbali za umma.
Mwenyekiti wa AAPAM Chapter Tanzania, Laila Mavika, anasema mada kuhusu tatizo la afya ya akili ilikuwa njema na kuwafungua masikio mameneja rasilimali watu wengi waliohudhuria kwani sasa wameongeza ufahamu wa namna ya kuwasiliana na jinsi ya kufanya kwa wafanyakazi wao wanapopatwa na tatizo hilo.
“Lengo la huu mkutano pamoja na mafunzo tuliyopeana ikiwemo tatizo la msongo wa mawazo na afya ya akili, lakini tumekutana kujadili changamoto zinazowakabili watumishi wa umma.
“Baada ya hiki kilichotokea kwenye mkutano huu matarajio yetu ni kwamba utakuwa msaada mkubwa kwa wataalamu wa utawala na rasilimali watu kwani ofisi zao ni chachu ya maendeleo katika taasisi zao,” anasema Laila.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chuo cha Uongozi, Kadari Singo anasema mafunzo hayo yamekuja wakati mwafaka kwani suala la afya ya akili na msongo wa mawazo ni tatizo kwa watu wa rika mbalimbali.
“Meneja rasilimali watu ni mtu muhimu na sisi huwa tunaangalia vitu mbalimbali kabla ya kutoa ajira… ndio maana wakati mwingine kwenye usaili unaweza kushangaa ukapewa mtihani wa kuandika na wa vitendo.
“Kwanini tunatoa mitihani wakati mwingine tunataka kuona je, uelewa wako uko vipi, unaweza kutenda ama kusema, kwa hiyo tunatazama mambo mengi kwa wafanyakazi kabla na baada ya kuwaajiri haya mafunzo pia yatasaidia, yatatuongezea kitu kwenye makabrasha yetu,” anasema Singo.
“Kwenye waliowasilisha mada hapa, nimeshangaa kusikia lawama kuelekezwa kwa meneja rasilimali watu kwamba wengine wana lugha zisizopendeza kwa watumishi, hili jambo halifai kwa ustawi wa taasisi. Yote haya ni ya kuyaangalia, meneja rasilimali watu ndio watu wa kwanza wanatakiwa kuwa na kauli nzuri kwa watendaji wao.
“Meneja rasilimali watu unakuwaje na lugha mbaya kwa wafanyakazi wako?
Wengine wanalalamikiwa wanakumbatia mafaili, kwa sababu gani? Wewe ni kiunganishi kati ya wafanyakazi na Mkurugenzi, unatakiwa kuwaunganisha taasisi badala ya kufanya mambo yaende tofauti. Watu watenge bajeti ya kutosha kuwafunza watu wao,” anasema Singo.
AAPAM Afrika ilianza mwaka 1962 kabla ya kuanzishwa Chapter Tanzania mwaka 2009 ikiwa na lengo la kuwawezesha viongozi hao kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Kila nchi ilianzisha tawi lake na kwa Tanzania, jumuiya hiyo inaratibiwa na kusimamiwa na Ofisi ya Katibu Mkuu katika Ofisi ya Rais, Menejimenti na Utumishi wa Umma na Utawala Bora kupitia Idara ya Rasilimali Watu.
Toka kuanzishwa kwake, wanachama wamefaidika kwa kuhudhuria mikutano mbalimbali Afrika.