MAMIA ya waombolezaji mjini Mbeya wamejitokeza katika mazishi ya wanandoa Grayson Ngogo(48) na mkewe Janet Luvanda(43) waliokufa katika ajali ya gari iliyotokea eneo la Iyovi mkoani Morogoro usiku wa kuamkia Desemba 26 mwaka huu wakitokea msibani Dar es Salaam.
Grayson ambaye alikuwa Makamu Mkuu wa chuo cha Ualimu St Agrey Mbeya na Janet aliyekuwa mwalimu wa Shule ya Sekondari Legico iliyoko Mbeya, walikuwa wanafuzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).
Wanandoa hao walioacha watoto wawili wa kike na wa kiume, walizikwa jana katika makaburi ya Nzovwe mkoani Mbeya huku ndugu wa upande wa mwanaume wakieleza kuwa kaka yao alikuwa tegemeo kwenye familia. Alisema kifo hicho kimewaachia pengo ambalo haliwezi kuzibika.
Ajali iliyosababisha mauti, ilihusisha gari ndogo aina ya Toyota Allion yenye namba IT 6954DNN, iliyogongana uso kwa uso na gari kubwa la mafuta aina ya Mercedes Benz lenye namba za usajili RAE 518C yenye tela namba RL 2686.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fortunatus Muslimu, katika ajali hiyo, watu watano wakiwamo wanandoa hao, walipoteza maisha.
Wengine ni Oswald Luvanda (42) ambaye ni kaka wa Janet, John Haule (37) ambaye ni mwalimu wa shule ya Wanging’ombe iliyopo mkoani Mbeya pamoja na Festo Sho aliyekuwa derava wa gari ndogo.
Katika maziko kwenye makaburi ya Nzovwe, mtoto wa kaka wa Grayson, Elesia Ngogo alisema siku aliyokufa baba yake mdogo huyo alikuwa anarudi kutoka kwenye msiba wa shemeji yake ambaye ni kaka wa mke wake.
“Baba yetu mdogo alikuwa ni msingi mkubwa katika hii familia aliishika hii familia, ndiye aliyekuwa anamlea mama yake ambaye ni mzee. Watoto wake aliowaacha wanasoma mmoja anaingia kidato cha tatu mwingine darasa la tano, tunaomba Mungu atushike,” alisema Elesia.
Maziko yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kiserikali akiwamo Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ambaye aliwataka waombolezaji kumtegemea Mungu na kuishi kwa upendo na mshikamano.
Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa Taasisi ya St Aggrey, Msajili kutoka Chuo cha Ualimu St Agrey Mbeya, Jeremiah Dennis, Grayson aliajiriwa na taasisi hiyo mwaka 2013 .
Licha ya kuwa makamu mkuu wa chuo hicho, alikuwa mkufunzi aliyebobea kwenye elimu ya mahitaji maalumu na kwamba taasisi imepoteza mtumishi hodari, mwadilifu na mchapakazi.
Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Legico, Martin Kalinga, alisema Janet aliajiriwa na serikali mwaka 2003 na alikuwa mwalimu mahiri wa Kiingereza ,mshauri kwa watoto wa kike katika Chuo cha Elimu ya Watu wazima tawi la Mbeya. Vile vile alikuwa mwezeshaji wa mtaala unaozingatia ujenzi wa umahiri wa somo la Kiingereza ngazi ya mkoa na kiongozi bora.