Man United mtegoni

MANCHESTER: WAKATI sikukuu za mwisho wa mwaka zikiendelea maeneo mbalimbali ulimwenguni michezo imekuwa ni sehemu ya kunogesha sherehe hizo.
Hekaheka za ligi mbalimbali zinaendelea ambapo katika Ligi Kuu ya England (EPL) michezo ya ligi hiyo pendwa ulimwenguni itapigwa hii leo, moja ya mchezo unaotizamwa kwa jicho la tatu usiku wa leo, Manchester United watakuwa nyumbani Old Trafford kuwaalika vijana wa Kocha Unai Emery, Aston Villa.
Mchezo huu unaonekana ni mkate mgumu kwa United kutokana na matokeo waliyopitia kwa michezo iliyopita wakiwa hawajashinda katika michezo minne iliyopita na ajabu zaidi hawajafunga bao lolote katika michezo hiyo.
Aston Villa wao wanapewa nafasi kubwa ya kuisambaratisha ngome ya Man United ikichagizwa na kiwango maridhawa walichonacho msimu huu wakitamba katika nafasi ya tatu na alama 39, wakitembeza vipigo kwa wakubwa na wadogo kumbukumbu nzuri wanayo Arsenal na Manchester City.
Villa hawajapoteza mchezo katika mechi 10 walizoshuka dimbani, mara ya mwisho kupoteza ilikuwa ni Novemba 05, 2023, walipofungwa 2-0 na Nottingham Forest.
Kwenye michezo saba ya mwisho timu hizo zilipokutana, Manchester United imeshinda michezo mitatu, Villa wakishinda michezo miwili huku sare zikiwa ni mbili ambapo jumla ya mabao 21 yamefungwa.
Michezo mingine ya EPL siku ya leo Newcastle United watakuwa wenyeji wa Nottingham Forest, Bournemouth watawaalika Fulham, Sheffield United Vs Luton Town na Liverpool watasafiri kuwafuata Burnley.

Habari Zifananazo

Back to top button