BONDIA Karim Said “Mandoga Mtu Kazi “, amesema kulala vizuri , lishe bora , mazoezi ya nguvu mara kwa mara imemuwezesha kuwa ni bondia wa kwanza nchini kupigana mapambano 16 mwaka uliopita.-
Mandoga alisema hayo mbele ya maelfu ya wananchi waliojitokeza kupokea eneo la Stendi ya Daladala ya zamani Manispaa ya Morogoro, wakati alipowasili jana akitokea jijini Dar es Salaam.-
Alisema kuwa mchezo wa ngumi kikanuni bondia anapaswa kucheza mapambano matatu tu kwa mwaka, lakini yenye kutokana na kulala vizuri , lishe bora anayoipata na mazoezi ya nguvu kila mara kumemwezesha kucheza mapambano hayo wa mwaka uliopita.
Alisema kuwa amepata umaarufu na mapokezi makubwa baada ya pambano lake na Mkenya Daniel Wanyonyi na hiyo ni kutokana na slogani yake ya ngumi ya kigeni anayoiita Sunguyo, ambayo ni ya hatari iliyomwadhibu bondia huyo Mkenya .
Aliushukuru ubalozi wa Tanzania nchini Kenya kwa kumpa mapokezi mazuri na Serikali ya Awamu ya Sita kwa kumpigania vizuri baada ya kupata ubingwa wake, ambapo amepokelewa vizuri jijini Dar es Salaam.
Aliwashukuru wananchi wa Mkoa wa Morogoroo kwa mapokezi mazuri waliyopatikana pamoja na viongozi wa serikali ya wilaya waliongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Albert Msando.
” Nilikaa na kusikiliza kweli mimi ni yatima niliyokosa baba na mama , bado sijamaliza kuwaza nikasikia simu Mandonga uko wapi nikajibu viongozi wangu wa Morogoro na kuwambia nipo Dar es Salaam , haraka sana urudi nyumbani kwako Morogoro ndugu zako wote wanakusubiri watu wanataka wakupokee wewe,”alisema Mandonga akielezea mawasiliano kwenye simu yake na viongozi wa Morogoro.
Alimshukuru Mungu kwa kila jambo, ambalo amemfanyia na kumuezesha kupata umaarufu na mapokezi makubwa ya wananchi wa Mkoa wa Morogoro.
Mapokezi makubwa ya bondia huyo yanaendeleza mwendelezo wa kuonesha upendo na kuwajali wasanii na wanamichezo wao, ambapo tukio kubwa lilianza mwaka 2002, ambapo Mwisho Mwampamba alikuwa Mtanzania wa kwanza kushinda shindano la Big Brother Afrika Kusini na alifanyiwa mapokezi makubwa ya heshima.
Mwaka 2004 msanii Selemani Msindi ‘Afande Sele’, akishinda ufalme wa Rhymes jijini Dar es Salaam na kupatiwa zawadi ya gari, aliporudi Morogoro alifanyiwa mapokezi ya kihistoria.
Mwendelezo huo ukijitokeza tena mwaka 2008 kwa Francis Cheka wa Morogoro alishinda mchezo wa ngumi jijini Dar es Salaam dhidi ya bondia mahiri Rashid Matumla .
Mwaka 2020 bondia Twaha Kiduku wa Morogoro alishinda pambano kubwa la ngumi mbele ya Dula Mbabe jijini Dar es Salam, alipewa zawadi ya gari na kama kawaida aliporudi Morogoro akafanyiwa mapokezi makubwa.