RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali imelitangaza eneo la Mangapwani kuwa la Bandari Jumuishi kwa shughuli za upokeaji na usafirishaji wa mafuta na gesi.
Dk Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 04 Februari, 2023 katika halfa ya ufunguzi wa mradi mkubwa wa ujenzi wa Bohari ya mafuta ikijumuisha miundombinu ya kupokea mafuta eneo la Mangapwani uliojengwa na kampuni ya United Petroleum (UP).
Dk. Mwinyi amesema lengo kuu la mradi huo ni kuwezesha kupokea meli kubwa za mafuta zitakazobeba mafuta ambayo yatatosheleza matumizi ya nchi kwa miezi mitatu.
Mradi huo mkubwa utaifanya Zanzibar kuwa lango la bandari kwa usafirishaji ambao utatoa huduma nchi za Afrika Mashariki na kusini mwa Afrika pia mradi huo utakuwa na bandari ya kisasa ya uvuvi na Chelezo.