Manispaa ya Iringa yapangua hoja za machinga

HALMASHAURI ya Manispaa ya Iringa imepangua hoja mbalimbali zilizotaka kukwamisha zoezi linalowataka machinga kuhama kutoka katika maeneo wanayolalamikiwa kufanyia biashara kwenda katika maeneo rasmi waliyopangiwa.

Wafanyabiashara hao wadogo walipewa hadi Machi 1, mwaka huu wawe wamehamia katika maeneo waliyotengewa baada ya Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) wa tawi la Iringa kutishia kutolipa kodi na ushuru wa manispaa kama machinga hao wataendelea kufanya biashara mbele ya maduka yao.

Katika kikao chake na JWT kilichofanyika mjini Iringa mwishoni mwa Januari 2023, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kihage alitoa mwezi mmoja kwa machinga hao wawe wameondoka mbele ya maduka ya wafanyabishara wengine na kuwataka watendaji wakuu wa manispaa hiyo kujitafakari kama zoezi hilo litashindikana.

Advertisement

Wakati siku za machinga hao kuhamia katika maeneo waliyopangiwa ya Community Centre, magari mabovu, zizi la ng’ombe na makaburi ya mlandege zikikaribia kumekuwa na mvutano miongoni mwa machinga hao wakiwemo wanaotoka kwenda katika maeneo hayo huku wengine wakigoma kwa madai ya kukosekana kwa baadhi ya miundombinu muhimu.

Miundombinu inayolalamikiwa na machinga hao hususani kukosekana katika eneo la makaburi ya Mlandege ni pamoja na vyoo, umeme na maji.

Akifungua kikao cha baraza la madiwani wa manispaa ya Iringa leo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa Ibrahim Ngwada alipangua hoja hizo akisema eneo hilo la makaburi ya Mlandege lipo karibu na soko jipya la Mlandege lenye vyoo 20 ambavyo vinaweza kutumiwa na wafanyabiashara hao wadogo pamoja na wateja wao.

“Kama mahitaji yatakuwa makubwa tuwahakikishie tutajenga vyoo vingine. Katika maeneo mengine nchini machinga wamehamia katika maeneo waliyopangiwa, ni sisi tu ndio tulikuwa tumebaki. Kwahiyo Machi 1, mwaka huu machinga wote wawe katika maeneo hayo,” alisema

Kuhusu umeme alisema wataangalia mahitaji ya umeme katika eneo hilo na kama mpango wa machinga hao ni kufanya biashara hadi usiku; “isiwe shida tutavuta umeme haraka iwezekenavyo.”

Kwa upande wa changamoto ya maji, Ngwada alisema huduma hiyo ipo na ni ya uhakika katika soko jipya la Mlandege na kwa kuanzia machinga hao wanaweza kuitumia wakati taratibu za kuwasogezea katika eneo lao zikiendelea.

Meya alizungumzia pia kitendo cha baadhi ya machinga kuvamia makaburi katika eneo hilo na kuanza kujenga vibanda vyao vya biashara akisema hakikuwa cha kiungwana.

“Tunashukuru suala hili tumelimaliza kwa busara baada ya menejimenti ya halmashauri kuingilia kati na machinga hao wanaotakiwa kujenga vibanda vyao nje kuzunguka makaburi hayo kusitisha mpango wao huo ambao kama ungeendelea ungesababisha taharuki kubwa,” alisema.