- Milioni 7 wana matatizo ya afya ya akili nchini
MATATIZO ya afya ya akili bado ni changamoto kubwa katika jamii ndio maana serikali inapambana kuhakikisha Watanzania wanaishi kwa afya bora na kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, takwimu za sasa zinaonesha Tanzania inakadiriwa kuwa na wagonjwa milioni saba wenye magonjwa mbalimbali ya akili huku zaidi ya watu milioni 1.5 wakiishi na ugonjwa wa sonona.
Kwa mujibu wa ripoti za afya ya akili za Wizara ya Afya, katika kipindi cha mwaka 2022/23 wagonjwa 138,625 wa afya ya akili wamepatiwa matibabu ya ugonjwa huo katika vituo mbalimbali vya afya nchini.
Akiwasilisha bungeni hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya 2023/24 ya Wizara ya Afya hivi karibuni, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema wizara imeendelea kuimarisha huduma za afya ya akili kwa kuendelea kujenga uelewa kwa jamii juu ya afya hiyo.
“Kazi kubwa iliyotekelezwa ni kuandaa kongamano na mdahalo wa kitaifa wa afya ya akili, uliofanywa Oktoba mwaka jana uliokuwa na lengo la kuleta pamoja wataalamu na jamii kujadiliana masuala ya afya ya akili kwa jamii, watoto, vijana na makundi mengineyo,” anasema Waziri Ummy.
Katika kongamano hilo wananchi 1,155 walishiriki huku wengine 8,150 wakishiriki kwa njia ya mtandao.
Anabainisha majukwaa huru matatu ya afya ya akili yameanzishwa kwa ajili ya kuendelea kutoa elimu kwenye jamii kuhusu afya ya akili na dawa za kulevya ambapo zaidi ya watu 10,000 wanashiriki kwenye kutatua changamoto za afya ya akili, ukatili na dawa za kulevya kupitia majukwaa hayo.
Anaongeza wizara imeendelea kuiwezesha Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, Dodoma kuendelea kutoa huduma bora za afya ya akili ikiwemo huduma za uchunguzi na tiba ambapo Sh bilioni mbili zimetolewa.
Ummy anasema, mwelekeo wa wizara ni kukusanya takwimu za wagonjwa wa afya ya akili wanaohudumiwa katika vituo vingine vya kutoa huduma za afya vya umma na binafsi.
Aidha, katika kuongeza wataalamu wa afya ya akili nchini, wizara inafadhili wataalamu 10 katika ngazi ya ubingwa wa magonjwa ya akili wanaosoma Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na inashirikiana na kuanzisha Programu ya Sayansi ya Saikolojia ngazi ya shahada.
Anasema uzalishaji wa wataalamu hao utatoa mchango mkubwa kuimarisha utolewaji wa afua za huduma ya afya ya akili nchini na wizara itaendelea kushirikiana na Muhas kutafuta rasilimali fedha ya kufadhili wataalamu zaidi.
Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu afya ya akili iliyochapishwa Juni 2022 ilionesha watu bilioni moja waliishi na matatizo ya afya ya akili mwaka 2019.
Aidha, asilimia 15 ya watu wazima wenye umri wa kufanya kazi walibainika kuwa na matatizo ya afya ya akili.
WHO inasema shughuli na kazi mbalimbali za binadamu huchangia kuongezeka kwa matatizo ya afya ya akili.
Shirika hilo linabainisha baadhi ya mambo yanayochangia pia matatizo ya afya ya akili ni ubaguzi na ukosefu wa usawa, uonevu na unyanyasaji wa kisaikolojia, unyanyasaji mahali pa kazi.
Ripoti hiyo inabainisha mambo hayo hayapewi nafasi ya kujadiliwa mahali pa kazi na hivyo kuendelea kuwa chanzo cha matatizo ya afya ya akili miongoni mwa jamii.
WHO imetoa mwongozo wa kukabiliana na changamoto hizo na kutaja njia bora zaidi za kushughulikia mahitaji ya wafanyakazi wanaopitia changamoto za afya ya akili na kupendekeza hatua za kuwasaidia ili kurejea kazini kwa walio kwenye hali mbaya.
Katika hilo, mwongozo huo unataka kuwepo na uingiliaji kati unaolenga kulinda afya ya akili ya wahudumu wa afya, wahudumu wa kibinadamu na wahudumu wa dharura.
Aidha, WHO na Shirika la Kazi Duniani (ILO), wamesema janga la Covid-19 duniani limesababisha ongezeko la asilimia 25 ya wasiwasi na msongo wa mawazo duniani kote.
Aidha, limesema serikali ambazo hazikujiandaa kukabiliana na janga hilo kwa upande wa afya ya akili ziliendelea kupata shida huku dunia ikiendelea kukabiliwa na uhaba wa rasilimali za kushughulikia athari ya afya ya akili.
Mwaka 2020, mataifa mbalimbali duniani yalitumia wastani wa asilimia mbili tu ya bajeti zao za afya kwa ajili ya afya ya akili, huku nchi za kipato cha chini zikitenga chini ya asilimia moja ya bajeti zake kwa ajili hiyo.
Shirika hilo limesema janga la corona limesababisha janga la kimataifa la afya ya akili, ambalo limesababisha kuwepo na matatizo ya afya ya akili kama vile msongo wa mawazo kwa mamilioni ya watu duniani kote.
Takwimu za WHO zinaonesha viwango vya wasiwasi pamoja na msongo wa mawazo viliongezeka kwa zaidi ya asilimia 25 katika mwaka wa kwanza wa janga hilo.
Wakati huohuo, huduma za afya ya akili zilitatizika na kwa hivyo kuwa vigumu kwa waathirika wengi kupata msaada.
Tatizo hilo linaonekana kuwa zaidi Afrika, ambako mtaalamu mmoja wa kiakili anahudumia watu 500,000. Idadi ambayo ni chini ya mara 100 ya pendekezo la WHO.
Shirika hilo linasema watu 11, katika kila watu 100,000 Afrika hujiua, ukilinganisha na watu tisa kwa kila watu 100,000 kwenye maeneo mengine duniani.
WHO inabainisha kuwa Afrika ina mataifa sita kati ya 10 duniani yenye idadi kubwa zaidi ya watu wanaojiua.
Mkurugenzi wa WHO Afrika, Matshidiso Moeti anasema uwekezaji wa kutosha unahitajika ili kukabiliana na tatizo la afya ya akili Afrika.
Comments are closed.