SERIKALI imetoa pikipiki 216 kwa maofisa ugani wa Mkoa wa Iringa, hatua itakayosaidia kumaliza kilio cha wakulima kutofikiwa kwa wakati na huduma za wataalamu hao katika kuiongezea tija sekta ya kilimo.
Akiwakabidhi pikipiki hizo katika hafla iliyofanyika mapema leo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Halima Dendego aliipongeza serikali ya Dk Samia Suluhu Hassan akisema:
“Inaonesha kwa vitendo jinsi inavyowajali wakulima na ndio maana inaendelea kusambaza vifaa hivi ili wafikiwe na huduma za ushauri kwa urahisi.”
Dendego aliwataka maofisa ugani hao kuzitumia pikipiki hizo kwa malengo yaliyokusudiwa na katika mkataba watakaoingia nao watalazimika kuwa na daftari litakaloonesha idadai ya wakulima waliowatembelea kila siku na huduma walizowapa.
Awali Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Iringa, Elias Luvanda alisema kabla ya pikipiki hizo 216, mkoa wao ulishagawa pikipiki zingine 15 kwa baadhi ya maofisa ugani.
Alisema kati ya pikipiki hizo 11 zilinunuliwa na halmashauri za wilaya, mbili na Tume ya Maendeleo ya Ushirika na nyingine mbili na Bodi ya Korosho Tanzania na hivyo kufanya jumla ya pikipiki zote kuwa 231.
Luvanda alisema mkoa wa Iringa una jumla ya maofisa ugani 230 wakati mahitaji yake ni 444 na hivyo kufanya uwe na upungufu wa maofisa ugani 214.
“Aidha tunaiomba serikali itenge fedha kwa ajili ya kuvifanyia ukarabati vituo vya ugani kwani kati ya vituo 18 tulivyonavyo, ni vituo viwili tu ndivyo vinavyofanya kazi,” alisema.
Luvanda alizingumzia pia changamoto zinazowakabili maafisa ugani hao kuwa ni pamoja na kutopata mafunzo rejea ili waongeze ufanisi na baadhi yao kukaimishwa majukumu mengine ya uongozi katika vijiji na hivyo kuzorotesha huduma zao kwa wakulima.