Maofisa ugani wapikwa mfumo wa CSDS

MAOFISA ugani zaidi ya 100 wa mikoa ya Iringa, Ruvuma, Rukwa na Katavi wanapata mafunzo ya uuzaji na ununuzi wa mazao ya chakula kupitia mfumo mpya wa kidigitali wa Crop Stock Dynamic System (CSDS) ambayo ni teknolojia inayotumika kusajili ghala, masoko na wafanyabiashara.

Mfumo huo unaolenga kuboresha ukaguzi na kufuatilia uhifadhi wa mazao ya kilimo kwenye ghala na yale yanayoingia sokoni unasaidia kuongeza ufanisi, kupunguza hatari, na kuboresha uzalishaji wa kilimo kwa kutumia teknolojia za kisasa za kidigitali na uchambuzi wa data.

Mratibu wa mafunzo haya yanayofanyika kwa siku tatu katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa mjini Iringa, Dk Abel Mtembeji alisema mfumo huo unatumiwa na wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabishara, wamiliki na waendeshaji ghala, na maafisa ugani-kutoa maamuzi

Alisema mafunzo hayo yatawawezesha maafisa ugani hao kujua namna ya kuchukua takwimu mbalimbali za mwenendo wa uuzaji na ununuzi wa mazao na kuziweka kwenye mfumo .

“Baada ya mafunzo haya maafisa ugani hawa watarudi makwao na kutoa mrejesho kwa wadau wakiwemo wa namna mfumo huo unavyofanya kazi na jinsi ya kuutumia kupitia program ya simu,” alisema.

 

Kabla ya kuanza kutumika kwa teknolojia hiyo ya utambuzi, Mtembeji alisema huko nyuma hawakuwa na takwimu sahihi kuhusu mazao na wapi yanapopatikana na badala yake walilazimika kutumia takwimu za jumla.

Kwa upande wao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamepongeza jitihada za Wizara ya Kilimo kwa kuanzisha mfumo huo wakisema umerahisisha kazi ya utumaji wa taarifa ukilinganisha na ilivyokuwa awali.

“Mfumo huu mpya utaenda kuongeza ufanisi katika utendaji wetu wa kazi tofauti na ilivyo kuwa hapo awali kwani umerahisisha utoaji wa taarifa za mwenendo wa bei za mazao sokoni kwa wakati,” alisema Afisa Kilimo wa Wilaya ya Iringa, Daudi Chilagane.

Chilagane alisema hapo awali wataalamu wa ngazi ya kata na tarafa walikuwa wanakusanya taarifa katika makaratasi kisha kuzituma wilayani jambo lililokuwa linachelewesha ukusanyaji wa taarifa hizo.

Aidha alisema kabla ya mfumo huo kuja ilikuwa ngumu kuwatambua na kuwadhibiti baadhi ya wafanyabiashara wanaouza mazao yaliyoharibika na kupoteza sifa ya kupelekwa sokoni.

Habari Zifananazo

Back to top button