Maofisa ugani watakiwa kutembelea wakulima

WADAU wa kilimo wameshauriwa kushirikiana kwa karibu kuwezesha wakulima kulima kilimo chenye tija kitakachoinua usalama na uhakika wa chakula pamoja na kuwapatia kipato.

Mratibu wa zao la mahindi kitaifa kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari), Kituo cha Ilonga kilichopo Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro, Dk Arnod Mushongi alishauri hayo alipozungumza na HabariLEO kuhusu dalili za ugonjwa wa mnyauko wa mahindi ulioonekana katika Kijiji cha Kwigutu, wilayani Butiama, Mkoa wa Mara.

Mushongi alisema endapo watafiti wa kilimo, maofisa ugani na wakulima watashirikiana, watatatua changamoto za magonjwa na wadudu zinazoathiri mazao. Alisema ugonjwa huo wa mnyauko wa mahindi unasababishwa na virusi na huweza kusababisha hasara ya asilimia 100 mashambani. Husababisha kuoza kwa punje za mahindi hivyo kuhatarisha ubora na usalama wa nafaka hiyo kwa chakula cha binadamu na mifugo.

Advertisement

Tangu kuingia kwa ugonjwa huo nchini mwaka 2012, alisema zimefanyika jitihada za kuutokomeza ikiwemo kutoa elimu kwa maofisa ugani, kampuni za mbegu, wadhibiti ubora wa mbegu, watafiti wa kilimo na wanataaluma.

Alishauri maofisa ugani kuwatembelea wakulima mara kwa mara wajue mipango yao kwa misimu inayofuata, pamoja na mbegu sahihi wanazopaswa kuzitumia na wawashauri. Mkulima Isaya Wambura kutoka Kijiji cha Kwigutu, Kata ya Masaba wilayani Butiama mkoani Mara alisema shamba lake la ekari mbili na nusu limeathiriwa na ugonjwa huo wa mnyauko wa mahindi.