MKURUGENZI wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Miriam Mmbaga amewataka maofisa utumishi na utawala kutoka wizara hiyo na taasisi zilizo chini yake kuwezesha watumishi walio chini yao kutekeleza majukumu yao vizuri, badala ya kuwasubiri wakosee ili kuwaadhibu.
Miriam alitoa kauli hiyo wakati akifungua mafunzo ya siku moja jijini hapa kwa maofisa utumishi na utawala kutoka wizara ya mambo ya ndani ya nchi na taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo.
“Kazi kubwa ya idara hizo ni kuhakikisha watumishi wanawezeshwa kutekeleza majukumu yao vizuri badala ya kuwasubiri wakosee ili kuwafungulia mashtaka.
“Idara za utumishi na utawala ndio zinazowezesha watumishi wengi kufanya kazi vizuri na kuiwezesha wizara kutimiza malengo yake. Sisi tuliopo wizara ya mambo ya ndani ya nchi tunawahudumia watumishi walio raia na ambao ni askari.”
“Hatuna budi kuhakikisha tunapata mafunzo ya mara kwa mara ili kupata ujuzi zaidi katika kushughulikia masuala ya kinidhamu ya watumishi na kutenda haki kwa mujibu wa kanuni na sheria zinazotuongoza katika kusimamia masuala ya kinidhamu,” alisema.
Miriam alisema katika kushughulikia mchakato wa mashauri ya kinidhamu ni vyema mamlaka za kinidhamu dhidi ya watumishi zinazingatia sheria za utumishi wa umma.
Kabla ya kuanzisha mchakato wa kinidhamu, uchunguzi wa awali unatakiwa ufanyike ili kuweza kujiridhisha kabla ya kufanya uamuzi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya maofisa utumishi, Ernajoyce Hallo kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Ally Shemahimbo kutoka Jeshi la Polisi walisema mafunzo haya ni muhimu kwani yatawajengea uwezo wa namna bora ya kushughulikia masuala ya kinidhamu ya watumishi ambayo yamekuwa yakijitokeza katika wizara.
Pia walisema mafunzo yatawasaidia kuwajengea uwezo, kuwashauri viongozi wao namna bora ya kuwasaidia watumishi na kuwachukulia hatua sahihi watumishi pindi wanapokuwa wamekosea bila kumwonea mtumishi na kutoathiri taswira ya taasisi.
Mkurugenzi Msaidizi Rasilimaliwatu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Hilda Tegwa alishauri kwamba baadhi ya sheria za kusimamia masuala ya kinidhamu ya watumishi zinatakiwa kufanyiwa marekebisho ili kuhakikisha zinakuwa na vifungu vya kuangalia usalama wao wakati wanaposimamia masuala ya kinidhamu.