‘Maombi mikopo ya halmashauri sasa kidijitali’

OFISI ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imewataka watendaji wa halmashauri zote nchini kuendelea kuhamasisha vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu kujisajili kupitia mfumo mpya wa maombi ya mikopo mtandaoni ili waweze kunufaika.

Akizungumza na HabariLeo, Mkurugenzi wa Idara ya Serikali za Mitaa katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Angelista Kihanga amesema mfumo huo ni rahisi kutumiwa na kwamba utasaidia kuondoa changamoto mbalimbali ikiwemo uwepo wa vikundi hewa, kukosekana uwiano wa mgawanyo wa asilimia za mikopo kwa vikundi na walengwa kujiandikisha zaidi ya kikundi kimoja.

Amesema kuwa amesema kuwa mfumo wa maombi ya mkopo wa asilimia 10 inayotolewa na halmashauri ni kupitia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) hivyo kwa kutumia simu janja au kompyuta mpakato, mwanachama anaweza kuingia kwenye mfumo huo.

“Kabla ya mfumo huu, vikundi vilikuwa vinapeleka maombi yao kwenye halmashauri kwa mkono.

“Takwimu zinaonyesha kwamba kabla ya mfumo utekelezaji ulikuwa ukikumbwa na changamoto kadhaa ambazo zimeondolewa baada ya kuanza kwa mfumo,” amesema Kihanga.

Ameeleza kuwa serikali kupitia Ofisa maendeleo wa Kata na vijiji wamekuwa wakihakikisha kwamba vikundi hivyo vinajisajili kwa kutumia mfumo huo kwa kwenda maeneo yenye mtandao yaliyopo karibu na maeneo wanayoishi.

”Asilimia 86 ya Watanzania wasiopata intaneti wako maeneo ya vijijini ikilinganishwa na asilimia 44.6 waliopo mijini lakini haizuii kutumika kwa mfumo huu kwa sababu maofisa maendeleo wanalazimika kwenda maeneo yenye mtandao ili kuvisajili vikundi hivi,” amesisitiza.

Pia amesema hatua za mwanachama au kikundi kusajili kupata mkopo kwa njia ya mfumo huo ni kufungua akaunti itakayomuwezesha kuingia kwenye mfumo na kwamba kiongozi wa kikundi ndiye anapewa jukumu la kuhariri taarifa za kikundi.

Mkurugenzi huyo amesema mfumo huo umesaidia kuimarika kwa usimamizi na ufuatiliaji wa marejesho na shughuli za vikundi kwa sababu ni rahisi kuwapata wanachama wote wa kikundi kupitia vitambulisho vya taifa (NIDA) ambavyo hutumika wakati wa usajili.

Vilevile ameeleza kuwa mfumo huo umeunganishwa na Wakala wa Serikali Mtandao (GePG) hivyo marejesho yote yanafanyika kupitia nambari ya udhibiti ambayo kikundi kinapatiwa na kulipa kwa kutumia mitandao ya simu, mawakala wa benki na benki.

“Vikundi vina uwezo wa kujua hali ya marejesho ya mikopo yao kupitia mfumo huu kwa kuwa kuna mfumo wa ufuatiliaji inayomuwezesha Ofisa maendeleo ya jamii kupata taarifa za kikundi kwa urahisi kwa sababu mfumo una taarifa za vikundi na idadi ya vikundi vinapopatikana nchini,” amefafanua.

Kihanga amesisitiza idara yake inaendelea kutoa elimu kupitia mafunzo kwa wakufunzi wa ngazi ya mkoa na halmashauri na wao kwenda kutoa mafunzo katika ngazi ya Kata na maofisa maendeleo ngazi ya kata hutoa mafunzo kwenye vikundi.

Habari Zifananazo

3 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button