Maonesho Fahari ya Geita yaiva

TAKRIBANI wajasiriamali 260 pamoja na wadau 56 wanatarajiwa kushiriki maonesho ya biashara ya Fahari ya Geita yanayofanyika kwa awamu ya nne katika halmashauri ya mji wa Geita mkoani hapa.

Mwenyekiti wa Kamati ya maonesho ya Fahari ya Geita, Mkurugenzi wa Kampuni ya African Creative, Raphael Siyantemi amebainisha hayo mbele ya waandishi wa habari kuelekea maonesho hayo.

Siyantemi amesema dhamira ya maonesho hayo kwa mwaka huu yanalenga kuhimiza maendeleo chanya katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kutanua wigo wa mapato kwa halmashauri na wajasiriamali.

Ameeleza, maonesho ya nne ya Fahari ya Geita yanafanyika chini ya kaulimbiu isemayo Kilimo, Ufugaji na Uvuvi Ni Nguzo Imara ya Maendeleo ya Mwananchi, Shiriki Kikamilifu Kuchagiza Ukuaji wa Sekta Hizo.

“Maonesho yatafanyika katika Uwanja wa CCM Kalangalala, na tunatarajia kwamba maonesho haya yatafunguliwa na Mkuu wa Mkoa, Martin Shigella na yatahitimishwa na Waziri wa Viwanda na Uwekezaji.

“Nitumie fursa hii kuwaomba sana, wafanyabiashara, wajasiriamali, na wadau wote waweze kujitokeza kwa wingi katika kuhakikisha kwamba wanapata matokeo chanya kupitia maonesho haya,” amesema.

Meneja wa Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) mkoani Geita, Nina Nchimbi amesema kupitia maonesho hayo SIDO wamejipanga kuongeza mwamko wa uongezaji thamani ya bidhaa za uvuvi, kilimo na ufugaji.

“Sisi kama Sido tayari tumeanza kutoa elimu wavuvi kidogokidogo na kuwaunganisha na taasisi zingine, ili kuhakikisha wanapata teknolojia nzuri na sahihi ya kukausha dagaa waweze kuwa na kiwango kizuri.

Amebainisha pia wamejipanga kuimarisha uvunaji wa mazao ya mifugo kutoka kwenye machinjio ya kisasa ya Mpomvu mjini Geita na kuwaelimisha wajasiriamali jinsi ya kuhifadhi na kusindika bidhaa za mifugo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Geita, Zahra Michuzi ameeleza maonesho hayo yatapanua wigo wa fursa kwa wajasiriamali hasa waliokopeshwa na halmashauri, ili kufikia azma ya kuzalisha kwa tija.

Zahra amewahakikishia washiriki wa maonesho ya Fahari ya Geita kuwa mazingira rafiki yameandaliwa kwa washiriki kutoka ndani na nje ya Wilaya ya Geita kuonesha ubunifu wao.

 

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x