Maonesho Juakali EAC yakonga mawaziri Tanzania, Uganda

WAZIRI Mkuu wa Uganda, Robinah Nabbanja na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Riziki Pembe, wameridhishwa na namna wajasiriamali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wanavyoongeza viwango vya ubora na ubunifu katika huduma na bidhaa wanazozalisha.

Walibainisha hayo wakati wakizungumza katika sherehe za ufunguzi wa Maonesho ya 22 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Wajasiriamali Wadogo na Wakati maarufu kama Juakali, zilizofanyika Desemba 11, 2022 katika Viwanja vya Uhuru vya Kololo jijini hapa.

Riziki alisema hatua iliyofikiwa na wajasiriamali hao ni dalili nzuri ya kufikiwa kwa lengo la kuyafanya maonesho ya Juakali kuwa jukwaa la fursa ya kukuza masoko, na kubadilishana uzoefu na teknolojia.

“Sote tumeshuhudia bidhaa mbalimbali zinazouzwa katika baadhi ya mabanda yaliyopo katika maonesho haya ambayo yamejumuisha nchi zote wanachama, bidhaa zina ubora na ubunifu wa hali ya juu,” alisema Riziki.

Akaongeza: “Hili la ubunifu na ubora wa bidhaa kila mwaka, ni dalili njema kwamba wana Afrika Mashariki tutakuwa na bidhaa zinazotosheleza mahitaji yetu kwa ubora na wingi hali itakayosaidia kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje.”

Katika maonesho hayo, imebainika kuwa, asilimia 87 ya wajasiriamali zaidi ya 300 kutoka Tanzania ni wanawake.

“Hii inadhihirisha kuwa, uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan unatoa kipaumbele kwa wanawake kwa kuzingatia kuwa mwanamke ni kiungo thabiti katika maendeleo ya familia na taifa kwa ujumla,” alisema Riziki.

Waziri Mkuu wa Uganda, Robinah Nabbanja aliyemwakilisha Museveni, alitoa mwito kwa serikali za EAC kuendelea kufanya mabadiliko muhimu kuhusu sera za uchumi ili kuleta msukumo, kuongeza uzalishaji wa bidhaa na kurahisisha zaidi ufanyaji biashara katika EAC.

“Kundi la wajasiriamali wadogo na wakati linachangia asilimia 60 ya pato la nchi wanachama wa EAC, huku asilimia 99 ya biashara ndogo na kati zikimilikiwa na wazawa wa Afrika Mashariki,” alisema Nabbanja.

Akaongeza: “Katika Waafrika 6 kati ya 10, wamejiajiri katika sekta ya biashara ndogo na kati, hivyo zinazalisha wastani wa ajira nane kwa kila ajira 10 mpya.”

Alisema sera zikiwa rafiki kiasi cha kutatua changamoto zinazowakabili wazalishaji wadogo, zitaleta manufaa kiuchumi kwa EAC kwa kuwa asilimia 99 ya wajasiriamali ni wazawa wa Afrika Mashariki.

Habari Zifananazo

Back to top button