Maonesho ya dawa kufanyika Dar
TANZANIA inatarajia kuwa mwenyeji wa maonesho ya sekta ya dawa na huduma za afya kwa wadau na wataalam wa afya kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Maonesho hayo yanatarajiwa kufanyika Desemba 14-16 mwaka huu, ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam, muandaaji wa maonesho hayo, Thomas James amesema yatatoa nafasi kwa Watanzania kubadilishana ujuzi wa dawa tiba na wataalamu wakubwa duniani.
“Maonesho yatawakutanisha wazalishaji, wauzaji wa jumla, wafanyabiashara na wasambazaji wa sekta ya uchunguzi wa dawa, hospitali na watoa ushauri wenye ushawishi mkubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki nchini Tanzania,” amesema.
Katibu Mtendaji wa MeLSAT, Peter William amesema kampuni zaidi ya 100 zitashiriki maonesho na kwamba katika kuhamasisha uwekezaji nchini kunahitaji kuwekeza kwenye viwanda hasa vya dawa.
Kwa upande wake Ofisa Mwanachama kutoka TWCC, Cresensia Mbunda, amesema kuwa maonesho yatasaidia kunufaika na kuongeza uwekezaji kutokana na ujuzi walioupata kupitia watu wa nchi mbalimbali.