Maonesho ya viwanda kuunganisha wawekezaji

KWA mara ya kwanza Tanzania imeandaa Maonesho ya Kimataifa ya wenye viwanda kwa lengo la kuunganisha sekta hiyo na wawekezaji kutoka nje ya nchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), Leodegar Tenga amesema hayo alipokuwa akizungumzia maonesho hayo yajulikanayo kama ‘ Tanzania International Manufacturers Expo 2023’.

Amesema maonesho hayo yanatarajiwa kufanyika kuanzia Oktoba nne mpaka sta mwaka huu jijini Dar es Salaam yameandaliwa na CTI kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara ( Tantrade).

“Maonesho haya ya wenye viwanda yanaashiria hatua kubwa ya maendeleo ambayo sekta ya viwanda na biashara imepiga hapa nchini,” amesema.

Amesema maonesho hayo yanatarajia kushirikisha wazalishaji wa bidhaa viwandani zaidi ya 500.

Pia amesema shughuli mbalimbali zitafanyika zikiwemo za uandaaji wa mikutano, semina, mijadala na hotuba mbalimbali kutoka kwa wafanyabiashara maarufu wa Tanzania na nje ya nchi.

Amesema maonesho hayo yataenda sambamba na utoaji tuzo za Rais wa 17 za wazalishaji bora wa mwaka.

“Maonesho haya pia yatatambulisha mifumo mipya ya biashara na teknolojia ya kisasa ili kuleta mafanikio makubwa katika sekta husika,” amesema.

Kwa mujibu wa Tenga maonesho hayo yatafanyika kila mwaka hivyo litakuwa jukwaa la pekee la kufikia maendeleo katika sekta ya uzalishaji wa bidhaa za viwandani na kuweza kupata soko nje ya nchi kwa kupitia muunganiko maalum utajaotokana na maonesho hayo.

Kwa upande wake Mratibu wa Maonesho hayo kutoka Tantrade, Fortunatuse Mhambe amesema taasisi hizo mbili zimeingia makubaliano hayo kuanzia mwaka huu na kuendelea.

Amesema wamejipanga kujenga mazingira maxuri ya sekta ya viwanda nchini ili kuleta maendeleo makubwa kupitia maonesho hayo.

Habari Zifananazo

Back to top button