HALMASHAURI ya Wilaya ya Nyang’hwale imeongeza asilimia 66.9 ya makusanyo ya mapato ndani ya miaka mitano, kutoka asilimia 54.3 mwaka 2018/19 na kufikia asilimia 121.2 kwa mwaka huu wa fedha.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita, Husna Toni amebainisha hayo wakati akizungumuza katika mkutano wa hadhara katika kijiji cha Nyijundu wilayani humo.
Amesema kwa mwaka wa fedha 2018/19 Nyang’ghwale ilipanga kukusanya kiasi cha Sh bilioni 1.4 na kufanikiwa kukusanya kiasi cha Sh milioni 759.9 sawa na ufanisi wa asilimia 54.3.
Amebainisha, kwa mwaka wa fedha 2019/20 halmashauri ilijiwekea malengo kukusanya kiasi cha sh milioni 832.19 na kufanikiwa kuvuka lengo kwa kukusanya Sh bilioni 1.01 sawa na ufanisi wa asilimia 121.9.
“Kwa mwaka wa fedha 2020/21 halmahsuari ilipanga kukusanya mapato ya Sh bilioni 1.5 lakini makusanyo yaliyofikiwa yaliyopatikana yalikuwa ni Sh bilioni 1.9 sawa na ufanisi wa asilimia 128.”
Ameongeza kuwa, kwa mwaka wa fedha uliopita (2021/22) walifanikiwa kukusanya jumla ya Sh bilioni 2.5 sawa na mafanikio ya asilimia 101.3 katika lengo lililowekwa la kukusanya Sh bilioni 2.4.
Husna amesema, kwa mwaka huu wa fedha hadi kufikiamwezi Mei 2023, wamekusanya sh bilioni 3.2 sawa na ufanisi wa asilimia 121.2 ikilinganishwa na lengo waliloweka la kukusanya sh bilioni 2.64.
Amefafanua, kati ya fedha iliyokusanywa mwaka huu wa fedha kiasi cha Sh bilioni 2.7 ni kutoka vyanzo vya ndani bila vyanzo lindwa huku Sh milioni 403.5 ikiwa ni mapato yatokanayo kwenye vyanzo lindwa.
Amesema, mbali na makusanyo hayo kwa mwaka huu wa fedha kuanzia Julai 2022 hadi machi 2023 wilaya hiyo imepokea jumla ya Sh bilioni 8.96 kutoka serikali kuu kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Wilaya inaendelea na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambapo miradi mbalimbali inaendelea kutekelezwa kwa fedha toka serikali kuu, wadau wa maendeleo na nguvu za wananchi.
” Ameeleza Husana.