Mapato ya uwekezaji yaing’arisha NSSF

MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba

MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba, amesema mfuko umepata matokeo makubwa na mazuri ya uwekezaji kutokana na kuwekeza kwenye maeneo salama. Mshomba alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya utendaji wa mfuko pamoja na vipaumbele kwa mwaka wa fedha 2022/23.

Alisema katika kipindi cha miaka miwili uwekezaji umeleta mapato makubwa ambayo hayajawahi kufikiwa; kwani NSSF haikuweza kupata mapato ya mwaka zaidi ya Sh bilioni 500, lakini katika mwaka huu wa fedha wamepata zaidi ya Sh bilioni 600.

Alisema matokeo hayo ya uwekezaji yametokana na mfuko kujikita zaidi katika uwekezaji kwenye maeneo ambayo yanaleta faida na kuhakikisha wanadhibiti fedha. Mshomba alisema chachu kubwa ya mafanikio ya NSSF yamechagizwa na kasi ya utendaji wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi makini wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Advertisement

“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa chachu ya mafanikio ya Mfuko wetu kutokana na kufungua fursa za uwekezaji,” alisema. Mshomba alisema katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2022 mfuko ulikusanya zaidi ya Sh trilioni 1.42 na kwamba makusanyo hayo ni zaidi ya bajeti ambayo walijipangia iliyokuwa ya Sh trilioni 1.38.