WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu, amesema ugonjwa wa saratani umekuwa tishio, ambapo kwa mwaka 2020 ulisababisha vifo vya watu zaidi 25,000, huku Covid 19 ikisababisha vifo visivyozidi 1000.
Waziri Ummy amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akizundua ripoti ya utafiti ya hali ya ugonjwa wa saratani Kusini mwa Jangwa la Sahara iliyofanyika mwaka huu, ambapo nchi za Afrika 46 zimeshiriki.
Amesema kutokana na utafiti huo, wamepokea mapendekezo nane, ili kupanga mipango ya kudhibiti saratani, ikiwemo kuboresha huduma za tiba na tiba shufaa kwa wagonjwa wa saratani.
Mapendekezo mengine aliyoainisha Ummy ni upatikanaji wa takwimu sahihi wa hali ya saratani, Kuweka mfumo mzuri wa kupata huduma bila kikwazo, kuboresha tiba, kuwekeza kwenye tafiti na ubunifu na kutengeneza wataalamu wazuri wa kutoa huduma bora .
“Taarifa hii inaonesha mzigo wa saratani unazidi kukua kwa kiasi kikubwa katika nchi zetu na wametoa mapendekezo ambayo tunapaswa tutekeleze kama nchi zetu, kubwa ni suala la takwimu nataka kusisitiza kwamba wanasema tunahitaji kuboresha upatikanaji wa takwimu kwa hali ya saratani katika nchi.
“Lakini pia wametoa ushauri wa kutengeneza mfumo mzuri wa watu kupata huduma bora za matibabu, bila changamoto ya fedha,”amesisitiza.