Mapitio Mitaala ya Elimu Msingi yakamilika
MAPITIO ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 na Mitaala ya Elimu Msingi yamekamilika na yanasubiri mchakato wa ndani ya Serikali ili kupata ridhaa ya rasimu zilizoandaliwa kupelekwa kwa wadau kwa mjadala wa kitaifa.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Profesa Adolf Mkenda wakati akizungumza katika Mahafali ya 41 ya Chuo Kikuu Huria Jijini Mwanza, ambapo amesema kuna mambo makubwa ambayo yamependekezwa na wadau mbalimbali.
Prof. Mkenda amefafanua kuwa utekelezaji wa kazi hiyo umeendelea kwa kushirikisha wadau mbalimbali wakiwemo Maaskofu, Mashekhe, walimu, wenye shule binafsi pamoja na wataalamu kutoka nje ya nchi ili kupata uzoefu kutoka katika nchi zilizoleta mageuzi ya elimu na kufanikiwa na zile ambazo hazikufanikiwa.
“Tumekamilisha rasimu ya mapitio ya Sera, ina mapendekezo mengi makubwa, tunachosubiri sasa ni mchakato wa ndani wa kupitia mapendekezo hayo kabla hatujayatangaza rasmi kwa ajili ya mdahalo wa kitaifa na hatimae mchakato wa maamuzi uweze kufikiwa ndani ya Serikali,” amesema Prof. Mkenda.
Akitolea mfano jambo moja ambalo limeguswa katika mapitio ya Sera ni suala la walimu kupewa kipaumbele katika ubora na suala mafunzo endelevu kazini. Hata sasa suala la mafunzo kazini limeshaanza na linaendelea.
“Katika mapitio ya Sera walimu waliopo wataendelea kupewa mafunzo kazini, ambayo tayari wameshaanza kuyapata na walimu wapya tutaona vigezo katika mapitio ya Sera kuhakikisha tunakuwa na walimu bora wa kuendeleza elimu yetu,” amefafanua Prof. Mkenda.
Amesema kuwa kazi ya kupitia mitaala nayo inakwenda vizuri pamoja na kuwa kwa kawaida hapa nchini kazi hiyo ilikuwa hailepelekwi katika ngazi ya maamuzi kutokana na kuwa ya kitaalamu zaidi, lakini kwa mageuzi haya ya elimu italetwa kwenye ngazi za juu na kisha kujadiliwa na umma wa Watanzania.
Ameongeza kuwa mageuzi hayo ya mitaala yatafanyika pia katika ngazi ya Elimu ya Juu ambapo huko utaangaliwa zaidi ubora wa elimu.