Maporomoko ya maji Kipengere yawewesesha watalii

ZAIDI ya watalii 200 kutoka mataifa mbalimbali wameadhimisha Siku ya Maporomoko ya Maji Duniani na kutalii kwa kuona vivutio vya utalii vilivyopo katika Pori la Akiba Mpanga/Kipengere lililopo chini ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).
Watalii hao waliambatana na Balozi wa Utalii nchini, Nicholas Reynolds maarufu Bongozozo ambaye pia ni mwanamitindo maarufu duniani.
Reynolds alitembelea hifadhi hiyo ikiwa ni ziara yake ya kuhamasisha na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Kusini mwa Tanzania pamoja na kuadhimisha siku ya maporomoko ya maji duniani inayofanyika kila Juni 16 ya mwaka na hapa nchini kitaifa yalifanyika katika pori hilo lililopo katikati ya mikoa ya Mbeya na Njombe.
Hiyo ni mara ya kwanza kwa Reynolds na wenzake kufika katika pori hilo na kusema alifurahishwa kuona mazao mapya ya utalii yaliyopo katika hifadhi hiyo.
Alisema “Tawa mserereko” ni zao la utalii linalomfanya mtalii kuburudika awapo katika hifadhi hiyo ambapo humfanya mtalii kuteleza katika maji jambo linaloleta furaha kwa mtalii.
“Nimetembelea maporomoko mengi sana hadi “Victoria Falls Zimbabwe’, maporomoko makubwa kuliko yote duniani lakini kumbe hapa ni tofauti sana,” alisema.
Reynolds maarufu kama Bongozozo aliipongeza Tawa kupitia uongozi wa Pori hilo kwa utunzaji mzuri wa mazingira na hivyo kuifanya hifadhi kuwa safi bila ya uwepo wa utupaji hovyo wa taka, jambo ambalo linavutia kwa kiwango cha juu watalii.
Akiwakaribisha watalii hao katika hifadhi hiyo, Kamishna wa Uhifadhi Msaidizi Utalii Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Martha Msemo alisema Pori la Akiba Mpanga/Kipengere limesheheni vivutio mbalimbali vya utalii wa kihistoria, utamaduni na mandhari mazuri kufanyika hifadhini humo.
Martha alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha miundombinu ya utalii katika pori hilo hususani malazi kwa wageni na watalii mbalimbali wanaotembelea pori hilo.
Akielezea umuhimu wa pori hilo alisema pori hilo la akiba lina vyanzo vingi vya maji ambayo kiikolojia yanatumika katika ikolojia ya Ruaha – Rungwa na pia maji hayo hutumika kuwasaidia wananchi katika shughuli za kilimo cha umwagiliaji.