Mapya: Simba waanza kufungiana

DAR ES SALAAM – SEKRETARIETI ya Klabu ya Simba imewafungia kujihusisha na masuala ya klabu hiyo wanachama Mohamed Khamis ‘Dk Mohamed’ na Agness Daniel ‘Aggy Simba’ mpaka pale Kamati ya Maadili iyakapoamua vingine.

Katika taarifa iliyotolewa jana na sekretarieti hiyo inasema wamepokea malalamiko mengi ya maadili dhidi ya wanafamilia hao ikiwemo kuitisha mkutano kinyume na taratibu na kuchochea migogoro ndani ya klabu.

“Sekretarieti itawafikisha wanachama hao mbele ya Kamati ya Maadili hivi karibunina uamuzi huo umefikiwa kwa mamlaka ya sekretarieti iliyonayo chini ya ibara ya 31 (4) g ya klabu ya Simba ya mwaka 2018 (kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2024,” ilisema taarifa.

Advertisement

Pia inasema ibara hiyo ni katika kuhakikisha mahusinano ndani ya klabu wanachama na mashabiki hayaathiriwi. Aidha sekretarieti inawakumbusha wanachama na mashabiki kuheshimu katiba, kanuni na miongozo iliyopo ndani ya klabu.

SOMA: Mfahamu msemaji mkuu mpya wa serikali

Simba inachukua uamuzi huo wa kuwafungia wanachama wake ikiwa ni siku kadhaa zimepita tangu muwekezaji wa klabu hiyo Mohamedi Dewji ‘Mo’ kutangaza kurejea kwenye nafasi ya Uenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu hiyo.

Kurejea kwa Mo kwenye nafasi hiyo kuliambatana na kujiuzulu kwa wajumbe wa bodi wa upande wake ambao ni Salim Abdallah ‘Try Again’, Dk Raphael Chegeni, Zulfikir Chandoo na Rashid Shangazi “Nimemuomba Mohamed Dewji arejee kuwa Mwenyekiti wa Bodi, mimi nimeamua kukaa pembeni lakini nitaendelea kuwa mwanachama hai wa Simba” alisema Try Again alipotangaza uamuzi wake wa kuachia ngazi kama Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Klabu hiyo.