Mara wataka majambazi washughulikiwe kimila

WAKAZI wa Kijiji cha Nyamakobiti, Kata ya Majimoto, mkoani Mara, wametaka warejeshewe madaraka ya kutumia mila na desturi zao katika kushughulikia wahalifu sugu, wakiwamo majambazi, ikiwa polisi watatishwa na maneno ya wanasiasa.

Hayo yameelezwa kupitia mkutano wa hadhara, ulioandaliwa na uongozi wa kijiji hicho, ili wajadili hali ya ulinzi na usalama wao, ikiwa ni wiki moja tangu watu watatu walioshukiwa kuwa majambazi, wauawe kwa risasi katika operesheni maalumu iliyofanywa na Polisi Mkoa wa Mara, Simiyu, Mwanza na Kanda maalumu ya Tarime/Rorya.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kitarahota B, Chacha Charles alisema licha ya tukio hilo, ujambazi bado ni changamoto kwao, wanahitaji operesheni za ulinzi ziendelee.

Leonad Renkerenge, alisema badala ya kumhangaisha Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camillius Wambura, waruhusiwe kutumia mila na desturi kama ilivyokuwa zamani, kushughulikia majambazi, ambao wanawafahamu kwa sababu wanaishi nao.

Bhoke Karogo (68) ambaye ni mlemavu wa macho, alisema Septemba 27 mwaka huu usiku, mlango wa nyumba yake ulivunjwa na wahusika walimuibia kuku 20, ambao aliwafuga kwa kipindi kirefu.

“Ilikuwa nikipata shida nauza kuku, najihudumia sasa wamewaiba wote,” alisema akishindwa kuzuia machozi.

Mkami Nyaitori mkazi wa Kitarahota A, alisema Septemba 26 mwaka huu usiku, watu walivamia nyumbani kwake wakiamuru awafungulie mlango, alinusurika kutobolewa usoni kwa kitu chenye ncha kali, wakati akiwachungulia dirishani.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kitarahota, Chacha Charles akizungumza kwenye mkutano huo. (Picha zote na Editha Majura).

“Waliniambia wangevunja mlango wangenichakaza na mtoto niliyekuwa naye ndani, sisi tukawa tunapiga mayowe,” alisema.

“Walijuaje naishi na mtoto peke yetu? Wahalifu bado tunao, naomba kila anayepokea mgeni ampeleke kwa mjumbe itasaidia,” alisema.

Manyenyere Enterenge (37) alitaka majukwaa ya kisiasa yasitumike kushambulia polisi katika mambo yaliyo wazi, alimuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuiongezea polisi nguvu, ili operesheni ziendelee, vinginevyo waachiwe jukumu la kushughulikia majambazi.

“Kijiji kinakosa maendeleo kwa sababu ya siasa, mbona hajawasemea Panya Road waliouliwa na polisi ina maana sisi hatuna thamani kama wanaoishi Dodoma au Dar es Salaam? Alihoji.

 

Bhoke Karogo

Aliwataka wanasiasa wanaolaumu polisi kwa vifo vya ndugu zao wanaotuhumiwa uhalifu wakumbuke na historia za hao wanaowatetea.

Habari Zifananazo

Back to top button