SERIKALI ya Marekani imeahidi kutoa kiasi cha Sh trilioni 1.17 (Dola milioni 500) kupitia Benki ya EXIM ya Marekani kuwezesha sekta ya usafirishaji, miundombinu ya teknolojia za kidijitali na nishati safi ili kukuza uchumi nchini.
Hayo yamesemwa leo Machi 30, 2023 Ikulu jijini Dar es Salaam na Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris amesema moja ya maeneo ambayo wamejadili na Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhimarisha ushirikiano na kuzindua ushirikiano mpya kwenye teknolojia ya 5G katika usalama wa mtandao.
“Ili kufanikisha hilo, nina furaha kutangaza mipango mipya, moja ya Marekani itaingia mkataba na Tanzania wa dola za Marekani milioni 500 ili kuwezesha kukuza biashara ya mauzo ya Marekani na Tanzania.
Amesema, lengo la kufanya kazi pamoja ni kuongeza uwekezaji wa kiuchumi nchini Tanania na kuimarisha uhusiano wa kiuchumi wa pande zote mbili.
Kamala amesema, katika suala la ukuaji wa uchumi, suala la utawala bora, utulivu na sheria rafiki, ndizo zinazovutia wafanyabiashara kuwekeza.Aidha, katika upande wa madini, amesema wanatarajia kujenga kiwanda kikubwa hapa nchini cha uchenjuaji wa madini yanayotumika katika betri za magari.