Marekani yawapongeza Samia, Mbowe
BALOZI wa Marekani nchini Tanzania, Michael Battle amewapongeza Rais Samia Suluhu Hassan na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa kutumia maridhiano kumaliza changamoto za kisiasa nchini.
Kupitia ukurasa wake kwenye mtandao wa kijamii wa twitter, Balozi Battle aliwapongeza viongozi hao kwa kuchagua maridhiano badala ya mgawanyiko na akaongeza kuwa walichokifanya ni ndicho kinachotakiwa katika siasa za kushinda bila uhasama.
“Tunaweza kujifunza kwa kilichotokea jana (juzi). Siku kubwa kwa demokrasia ya Tanzania,” alieleza.
Awali Balozi Battle alieleza kuwa jambo kubwa la kwanza kuwewezesha wanawake kuingia kwenye nafasi za uongozi ni kuwapa mifano ya wenzao waliofanikiwa na kuonesha njia.
Juzi Rais Samia alizungumza katika mkutano wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) kusherehekea Siku ya Wanawake Duniani na akasema linajengwa taifa jipya la Tanzania lenye ushindani wa kisiasa bila vurugu.
Alisema mjini Moshi kuwa tukio la yeye kuhudhuria mkutano huo haijapata kutokea katika historia ya nchi hii na ni faraja kwake.
Rais Samia alisema sababu za kuhudhuria kwenye kongamano hilo ni kwa kuwa yeye ni Rais wa makundi na vyama vyote nchini na alitamani kusikia Chadema wanataka nini na alibuni maridhiano ili kuliunganisha taifa.
‘’Tuache kuvutana pasipo sababu kama kuna hoja basi tukae chini tuzungumze na sio kushambuliana kwenye majukwaa na ndio maana naunga mkono slogan yenu ya never, never again. Tusirudi tulipotoka bali tulenge kustawisha jamii ya Watanzania kwa kuwa na siasa za kistaarabu,’’ alisema.
Rais Samia alisema kukitokea vurugu za kisiasa wanaoumia ni wanawake na watoto hivyo wanawake wahakikishe nchi inabaki salama.
‘’Wapo watu ambao wanapinga hatua hii kati yangu na Mwenyekiti wa Chadema, si rahisi utamaduni huu kukubalika. Nasoma maoni yenu mtandaoni nacheka….sio rahisi kukubalika na wote lakini wakiona matunda chanya watakubali, lengo letu ni kujenga amani,’’ alisema.
Rais Samia alisema nchi itaendelea kuwa na mazungumzo na maridhiano endelevu ili kudumisha amani na utulivu ili kuleta maendeleo.