Marobota 600 vitenge yadakwa bandari bubu

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa Kigoma kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama wamekamata marobota 600 ya vitenge vilivyoingizwa nchini kwa njia za magendo.

Kaimu Meneja wa TRA wa mkoa huo, Deogratius Shuma alisema vitenge hivyo vilishushwa kwenye bandari isiyo ya rasmi kwenye ufukwe wa kijiji cha Kabeba wilayani Uvinza mwambao wa kusini wa Ziwa Tanganyika.

Shuma aliwaeleza waandishi wa habari kijijini hapo kuwa wamiliki wa vitenge hivyo hawajafahamika na pia thamani ya mali hiyo bado haijajulikana na kwamba, vilianza kushushwa kutoka kwenye boti usiku wa kuamkia juzi na kuhifadhiwa kwenye nyumba ambayo haijakamilika.

Alisema vitenge hivyo vitahamishiwa Kigoma mjini umbali wa kilometa 40 kutoka kwenye bandari hiyo bubu.

Mkuu wa Mkoa Kigoma, Thobias Andengeye alilaani wafanyabiashara wanaojihusisha na uingizaji bidhaa kwa njia haramu.

Andengeye alisema uchunguzi unaendelea na muda si mrefu wahusika watabainika na akasema serikali ya mkoa huo kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama wameimarisha ulinzi na doria kwenye bandari bubu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Filemon Makungu alisema wameanza kuchunguza ili kuwatambua wamiliki wa vitenge hivyo.

Alisema katika marobota hayo yapo majina ya baadhi wafanyabiashara wa vitenge katika soko la Kigoma ambao wanajulikana hivyo uchunguzi utawezesha kuelewa uhusiano wa majina hayo kwenye marobota hayo na umiliki wake.

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button