Marubani wasinzia ndege ikitua

Shirika la ndege la Ethiopia

MARUBANI wawili wamejikuta wamelala wakati ndege ikiwa juu umbali wa futi 37,000 (11,000m) na kuipita njia ya kurukia na kutua ndege kabla ya kuamka na kutua kwa usalama, chapisho la anga linasema.

Waongoza ndege katika uwanja huo, walijaribu kuwasiliana nao baada ya kuvuka eneo la kuteremka kwenye uwanja wa ndege wa Addis Ababa nchini Ethiopia. Hata hivyo, marubani hao hatimaye waliamka na kutua ndege katika njia yake ya pili, shirika la Aviation Herald lilisema.

Wafanyakazi wa shirika la ndege la Ethiopia wamepewa likizo kusubiri uchunguzi, chombo cha habari cha serikali cha Fana kiliripoti. Ndege ya shirika hilo ya abiria, iliruka kutoka uwanja wa ndege wa Khartoum, Sudan. Ndege hiyo aina ya Boeing 737 yenye uwezo wa kubeba abiria 154, kwa kawaida huchukua chini ya saa mbili katika safari yake kwenda na kutoka nchi jirani.

Advertisement

“Nisengetupia lawama wafanyakazi wa Ethiopia haswa hapa, hili ni jambo ambalo linaweza kutokea kwa wafanyakazi wowote duniani na pengine lawama ziko kwa shirika na wasimamizi,” mmoja wa waliotoa maoni alisema. Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Shirika la Ndege la Ethiopia lilithibitisha kuwa wafanyakazi hao walikuwa wameondolewa kwenye safari za baadaye kusubiri uchunguzi zaidi.

“Hatua stahiki za marekebisho zitachukuliwa kulingana na matokeo ya uchunguzi. Usalama umekuwa na utaendelea kuwa kipaumbele chetu cha kwanza,” ilisema taarifa hiyo.