WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angeline Mabula amewataka wananchi wanaokabidhiwa hatimiliki za ardhi kuhakikisha wanazingatia masharti yaliyopo kwenye hati sambamba na kufuata mipango kabambe ya maeneo husika.
Dk Mabula amesema hayo eneo la Shibula wilayani ilemela mkoani Mwanza, wakati wa kutoa hatimiliki za ardhi kwa wananchi wa eneo hilo. Jumla ya Hati 570 ziliandaliwa kwa ajili ya kuwapatia wananchi wa eneo hilo.
‘’Huwezi kupata hati leo, kesho unaenda kuomba kubadili matumzi mwisho wake miji inaonekana haina maana na haipendezi na sisi tunataka Jiji la Mwanza na Ilemela ikiwemo liwe mfano, tunapima viwanja vingi kwa ajili ya uwekezaji tuzingatie kilichopo kwenye Master Plan,’’ alisema Dk Mabula.
Amewaonya wanaopata hati milki za ardhi kutobadili matumizi na kuwaagiza watendaji wa sekta ya ardhi na uongozi wa Wilaya ya Ilemela kuhakikisha hakuna kubadili matumizi na badala yake wamiliki wazingatie masharti ya hati na yale matumizi yaliyopo kwenye mpango kabambe.
Akigeukia suala la utoaji hatimiliki za Ardhi katika halmashauri ya Manispaa Ilemela, Dk Mabula ameshangazwa na idadi ndogo ya wamiliki waliojitokeza kuchukua hati ambao ni 50 kati ya 570 walioandaliwa kuchukua hati.
‘’Watu wana tabia ya kulalamika hati hazitoki, tuna hati 570 hapa waliojitokeza ni 50 tu, hao wengine wako wapi ni kitu ambacho hakieleweki, hati zinaandaliwa lakini hamji kuchukua, hizo zinazobaki naomba muangalie namna mtakavyotoa,” alisema Dk Mabula
Ametaka wamiliki wa ardhi walioshindwa kuchukua hati kuandaliwa utaratibu maalum wa kupatiwa hati hizo huku akieleza kuwa, idara ya ardhi katika halmashauri ya Ilemela kwa kushirikiana na ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mwanza kuchagua sehemu moja na kutumia wiki mbili kutoa hati kwa wahusika ili ziweze kuisha na kuendelea na hati nyingine ambazo ziko katika mchakato.
Ameeleza kuwa wizara yake iko katika mageuzi makubwa ya kubadilisha mifumo yake, lengo likiwa kuweka taarifa za ardhi sawa, kuondoa migogoro ya ardhi pamoja na kuwezesha serikali kukusanya mapato yatokanayo na kodi ya pango la ardhi.
‘’Mifumo inaboreshwa na taarifa za sekta ya ardhi zinaenda kukaa vizuri na sasa taarifa ya kudaiwa kodi ya ardhi utaipata kupitia simu yako ya kiganjani na unapopata ujumbe nenda kalipe maana huhitaji kwenda ofisni,’’ alisema Dk Mabula
Kufuatia hatua hiyo, Dk Mabula aliwataka watendaji wa sekta ya ardhi kutimiza majukumu yao na kusisitiza kuwa asingependa Watanzania wenye shida kwenda ofisi za ardhi na kuelezwa njoo kesho na kuweka bayana kuwa kama suala haliwezekani ni bora kuelezwa ukweli.