Marufuku tumbaku kuuzwa kampuni zisizo na leseni

Marufuku tumbaku kuuzwa kampuni zisizo na leseni

BODI ya Tumbaku Tanzania (TTB), imewaagiza wakulima wa tumbaku katika maeneo yote yanayozalisha zao hilo nchini kutouza zao hilo la kimkakati kwa kampuni zisizo na leseni za kununua bidhaa hiyo.

“Wakulima msiuze tumbaku kwa makampuni ambayo hayana leseni ya kununua tumbaku kutoka TTB na bodi itatoa maelekezo haya kwa wakulima wote nchini,” alisema Mkurugenzi Mtendaji TTB, Stanley Mnozya.

Aliyasema hayo kwenye mkutano wa wadau wa tumbaku uliofanyika mjini Iringa na kujadili changamoto na upangaji wa madaraja ya tambaku. Mara ya mwisho mkutano kama huo ulifanyika mwaka 2011.

Advertisement

Mnozya amezitaka kampuni zilizopata leseni za kununua malighafi hiyo inayotumika kutengenezea sigara kupitia vyama vya ushirika.

“Bodi imetoa leseni za ununuzi kwa baadhi ya kampuni na zipo kampuni nyingine ziliomba leseni, lakini hazikupata, kampuni hizo zitambue zimekosa leseni kwa sababu hazijakidhi vigezo hivyo, wakulima wasiuze tumbaku kwao,” alisema.

Pia aliwaomba wakulima kuhakikisha wanang’oa mabua ya tumbaku mashambani, kabla ya kuanza masoko na kuongeza kuwa vyama vya msingi ambavyo wakulima wake hawatatekeleza agizo hilo masoko yao hayataanza.

Alisema hatua ya kung’oa mabua inalenga kupuungza  wadudu na usugu wa magonjwa kwa zao  hilo.

Mnozya alisema tumbaku ni zao la serikali la kimkakati linalochangia kwa kiasi kikubwa fedha za kigeni na pato la taifa.

Ameiomba serikali kupitia mfumo wake wa usambazaji pemebejeo kwa wakulima uwe kwa wakati, ili kuwawezesha kuzalisha kwa tija.

TTB pia imewataka wakulima na wadau mbalimbali wa tumbaku kuendelea kupanda miti kwa wingi, ili kulinda mazingira, kwani ukaushaji wa tumbaku unatumia zaidi nishati ya kuni.

Akifungua mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Halima Dendego aliwataka wanunuzi wa zao hilo kufanya biashara kistaraabu na kizalendo kwa kununua kwa bei inayoendena na masoko ya kimataifa ili wakulima nao wapate faida.

Alisema yapo makampuni yanayolalamikiwa sana na wakulima kuwanyonya kwa kununua zao hilo kwa bei ndogo ambayo aiendani na soko.

Alisema wanunuziwakinunua tumbaku kwa bei nzuri itawafanya wakulima waeendelee kuwa na moyo wa kuzalisha kwa tija na kwa wingi zaidi.

“Wanunuzi msiwakatishe tamaa wakulima, wakulima wakiacha kuzalisha kwa sababu ya bei ndogo hiyo ni hasara kwa kampuni zenu, viwanda na ni changamoto kwa ajira za watu wetu,” alisema.

Alisema ili kuwepo na uzalishaji endelevu wa tambaku, lazima mnyororo wa thamani wa zao hilo uwekewe msukumo mpya na akawataka wataalamu na maofisa kilimo mkoani humo kufuatilia uzalishaji wake ili kuweza kuuweka mkoa katika ramani.

Pia Dendego amewataka wakulima mkoani Iringa kuongeza uzalishaji wa zao hilo kama mikoa mingine akisema takwimu zinaonesha ni wa mwisho kwa uzalishaji pamoja na uwepo wa ardhi ya kutosha na hali ya hewa nzuri.

Mbali na Iringa mikoa mingine inayozalisha tambaku ni  pamoja na Ruvuma, Katavi, Mbeya, Tabora, Kigoma, Shinyanga, Singida, Mara, Geita, Kagera na Morogoro.