Marufuku vimemo ajira mpya 21,000

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Angellah Kairuki amesema ajira 21,000 za kada ya ualimu na afya watatenda haki na kwamba hatofanyia kazi vimemo vinavyotolewa na baadhi ya viongozi.

Pia amesema  mtumishi yeyote wa Tamisemi atakayebainika kuchukua rushwa au kufanya upendeleo wa aina yoyote katika kutoa ajira hizo basi atachukuliwa hatua kali za kinidhamu.

Kairuki ameyasema hayo leo Aprili 18, 2023 akihitimisha majadiliano ya bajeti ya wizara yake.

“Tutahakikisha zoezi hili linaenda kwa haki, wapo viongozi walionipigia simu na wengine kunitumia meseji wala sijajibu, tutatenda haki, bila hivyo tutawanyima haki watu wasiokuwa na viongozi wa kuwasemea, hata mimi nina ndugu zangu, lakini nimewambia waende kwenye mfumo rasmi,” amesema.

“Hata kama kuna mtumishi Tamisemi atakayefanya vitendo vyovyote vya ukiukwaji haki atakwenda na maji, ndio maana kila siku natoa matangazo katika hili hakuna rushwa. Mfumo utafungwa tarehe 25.”

Aidha, amesema hoja ya walimu wanaojitolea serikali inatambua wapo walimu na watu wa afya wanaojitolea.

“Tunatambua uwepo wa walimu wanaojitolea kwa shule za msingi na sekondari, na uwepo wa walimu umesaidia kupunguza changamoto ya walimu katika baadhi ya maeneo  nchini.

“Hadi sasa hatuna mfumo rasmi unaotumika kuwatambua wanaojitolea, baadhi ya walimu walikuwa wanapata nafasi ya kujitolea lakini wapo wanaotamani kuipata lakini wameikosa, hali kadhalika kwenye kada ya afya.

“Kukosekana kwa mfumo rasmi bado unaweka ombwe kati ya walimu na sekta ya afya na kituo ambacho wanajitolea….

“Tunaandaa mfumo wa elekroniki kuona namna gani waombaji waombaje, Kanzi Data itakuwaje, utendaji wao na ufuatiliaji….mfano Kinondoni wameomba 150 wamepata 50 tu , katika hili katika mchakato huu tutaanza na waliomaliza vyuo mwaka 2015,”amesema.

Habari Zifananazo

Back to top button