KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi amepiga marufuku watoto wadogo kuanzia umri wa miaka mitatu hadi minane kupelekwa kwenye vibanda vya kuonesha video katika msimu wa Sikukuu ya Pasaka.
Akizungumza na HabariLEO jana alisema baadhi ya mabanda ya video yamekuwa yakionesha video ambazo hazina maadili kwenye jamii.
Kamanda Magomi alisema lengo la kupiga marufuku watoto wasiende kwenye vibanda vya video ni watoto kuanza kujifunza vitendo viovu katika umri mdogo.
“Ulinzi na usalama kwa watoto ni muhimu inatakiwa wazazi na walezi kukomesha vitendo viovu kwa kuanzia kwenye ulinzi wa mtoto na kile anachojifunza,”alisema.
Kamanda Magomi alisema jeshi la polisi limeimarisha ulinzi kuanzia kipindi chote cha Sikukuu ya Pasaka kuhakikisha watoto wahazururi hovyo na kwenda kwenye mabanda ya video.
Mwanasheria Felix Ngaiza kutoka shirika la kupinga Vitendo vya Ukatili Aids Control Programu (Agape) lililopo wilayani Shinyanga alisema suala la ulinzi na usalama kwa watoto linahitaji umakini mkubwa kwa kushirikiana na wamiliki wa mabanda hayo wazazi na vyombo vya usalama.
Ngaiza alisema ipo sheria ya mtoto ya mwaka 2009 namba 21 lengo lake mtoto kuwa katika mazingira ya Ulinzi na kubaki akiwa salama.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mitimirefu, Nassor Warioba alisema wako tayari kushirikiana na jeshi la polisi katika msimu huu wa sikukuu ya Pasaka kuwalinda watoto dhidi ya vibanda vinavyoonesha video zisizo na maadili ni njia mojawapo ya kuharibu watoto.
Baadhi ya wazazi manispaa ya Shinyanga Joramu Musa na Selina Rugobi walisema vibanda vya kuonesha video vipigwe marufuku na kuhoji video zinazooneshwa zinahakikiwa na nani na watoto wanapenda kuangalia ili mradi video imewekwa.