Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amesema nchi iko salama huku akiwasihi wananchi kuendelea na shughuli zao.
Hata hivyo, Masauni amesema Jeshi la Polisi linaendelea na operesheni ya kumaliza vitendo vya kihalifu.
Waziri Masauni ameyasema hayo leo, Septemba 16 l, wakati wa mkutano wake na wandishi wa habari juu ya hali ya usalama nchini huku akiwaahidi Watanzania kuwa serikali itaedelea kuwasaka wahalifu pamoja na wanaoshirikiana nao.
“Hakuna mtu yoyote atakayejihusisha na uhalifu na akabaki salama. Wote tutawakamata pamoja na wanaowasaidia na wanaonunua bidhaa za wizi na kuwafikisha katika mikono ya sheria,” amesema Waziri Masauni.
Katika mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na Naibu Waziri wake, Jumanne Sagini pamoja na Inspekta Jenerali wa Polisi (IJP), Camilus Wambura pamoja na wakuu wa vyombo vingine vya ulinzi na usalama.
Kwa upande wake IJP Wambura ametoa onyo vya vikundi vyote vya uhalifu huku akisisitiza Jeshi hilo halijawahi kushindwa na mhalifu yoyote.
Ameongeza kuwa Jeshi la Polisi limeshaanza operesheni huku akiwataka wazazi kuhakikisha wanafuatilia nyendo za watoto wao.