Mashabiki 48,000 kuingia bure Yanga Vs Mamelodi

DAR ES SALAAM: MENEJA Habari na Mawasiliano wa Yanga SC, Ali Kamwe amesema mashabiki 48,000 wataketi bila kiingilio kushuhudia mchezo wa kimataifa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL) Yanga dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Akizungumza leo katika ofisi za Makao Makuu ya Yanga, mtaa wa Twiga, Kariakoo Dar es Salaam, Kamwe amesema mchezo huo utakaopigwa Machi 30, mwaka huu  Uwanja wa Benjamin Mkapa, utaruhusu mashabiki hao kuketi katika majukwaa ya mzunguko na machungwa.

Akihamasisha mashabiki kujitokeza kushuhudia mchezo huo wa kihistoria, Kamwe amesema viingilio vitahusisha tu majukwaa ya hadhi ya VIP A, Sh 30,000 VIP B Sh 20,000 na VIP C, Sh 10,000.

Advertisement

“Viongozi wa klabu yetu hawana tamaa ya fedha, ndio maana tumepunguza na kuondoa tiketi ya mzunguko kwa lengo la kuhakikisha wengi waje uwanjani.

“Tumeweka maslahi ya mpira wa Tanzania mbele. Mechi ya Mamelodi ni kubwa mno lakini kwa kuwa lengo sio fedha ni hamasa basi tunawasihi mashabiki kujitokeza kwa wingi. Kiasi cha fedha ambacho ungelipia tiketi ya mzunguko basi utatumia kama nauli ya usafiri wa kukufikisha uwanjani na baada ya mchezo wetu uweze kurudi nyumbani salama,” amesema Ali kamwe