Mashabiki wa Simba Mtegu waanza kutamba

USAJILI uliofanywa na Simba SC kwa kuwachukua wachezaji 10, huku ikimrudisha winga Luis Miquissone umeanza kuwapa jeuri baadhi ya mashabiki wa timu hiyo kuekea msimu mpya wa ligi.

Mashabiki wa wapenzi wa timu hiyo kutoka kijiji cha Mtegu Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara wamesema msimu huu wanamatumaini makubwa na timu yao kufanya vizuri kwa kuwa imefanya usajili wa uhakika wa kuwapata wachezaji bora na wenye viwango vya hali ya juu.

Advertisement

Akizungumza wiki hii wakati wa uzinduzi wa tawi la timu hiyo katika eneo hilo hapo mwenyekiti wa tawi hilo, Ismaili Mkweche amesema tawi hilo lina wanachama 288 na limefunguliwa kupitia michango mbalimbali kutoka kwa wanachama hao.

Amesema kutokana na kiu kubwa waliyokuwa nayo wanachama wa timu hiyo kijijini hapo ya kupata tawi lao hivyo walichangishana na kufanikiwa kukusanya zaidi ya Sh milioni 3.

Shabiki wa timu hiyo kijijini hapo Zakia Selemani amesema: “Naipenda sana timu yangu ya simba na napenda kuwatia hamasa watu wote popote pale walipo waje kushabikia tawi la mtegu hata wale wasiyokuwa mashabiki wa Simba.”

Msemaji wa matawi ya simba Kanda ya Kusini, Zuberi Mohamedi amesema wana imani na timu yao na katika kipindi hiki (Simba Day) watatembelea tawi hadi tawi kwenye maeneo mbalimbali mkoani humo.

Amesema uzinduzi huo ni hatua ya awali na kwenye wiki hiyo watafanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo uchangiaji wa damu na wanatarajia kuzindua matawi manne ndani ya wiki hiyo.

Uzinduzi huo umefanywa na Mwenyekiti wa simba kanda ya kusini Baraka Namkutanga ambapo amewapongeza mashabiki hao kwa uwamuzi waliyochukua kuanzisha tawi hilo.

6 comments

Comments are closed.