Mashahidi 28 kesi mauaji ya mke na kuchoma maiti yake
UPANDE wa mashitaka (DPP) katika kesi ya mauaji inayomkabili mfanyabiashara Khamis Luwonga (38) anayetuhumiwa kumuua mke wake Naomi Marijani na kisha kuuchoma mwili wake moto kwa kutumia magunia ya mkaa imeileza mahakama ya hakimu mkazi kisutu kuwa watakuwa na mashahidi 28.
Hayo yameelezwa juzi na Wakili wa Serikali, Mosie Kaima mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Ramadhani Rugemalira kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kumsomea mshtakiwa maelezo ya mashahidi.
Kaima alieleza mahakamani hapo kuwa pia watakuwa na vielelezo 14 kati ya hivyo vielelezo saba ni nyaraka na vingine ni vielelezo vingine halisi.
Kaima aliieleza mahakama kuwa miongoni mwa mashahidi hao ni madaktari, ofisi ya mkemia mkuu, askari polisi, mlinzi wa amani na baadhi ya ndugu wa marehemu.
Kwa upande wake mshtakiwa amedai kuwa anatarajia kuleta mashahidi 20.
Katika kesi hiyo inadaiwa kuwa Mei 15, mwaka 2019 eneo la Gezaulole eneo Kigamboni Khamisi alimuua Naomi Marijani na kisha kumchoma moto kwa kutumia magunia mawili ya mkaa
Kesi hiyo imeahirishwa hadi itakapopangiwa tena kikao mahakama kuu.