Mashindano ya Kata kwa Kata Dom yaja

BAADA ya kumalizika kwa mashindano NDONDO CUP DODOMA 2022  kwa mafanikio makubwa,sasa Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Anthony Mavunde ameweka nguvu kwenye mashindano ya mpira ya kata kwa kata Jijini Dodoma.
Akizungumza katika  fainali za mashindano ya Kombe la Iyumbu zilizofanyika jana Oktoba 2, 2022 katika viwanja vya shule ya msingi Iyumbu,Jijini Dodoma, Mavunde alisema ameona  umuhimu wa kuwa na mashindano hayo ya Vijana katika kata zao.
Michezo sio burudani peke yake,michezo ni ajira, lazima tutumie mashindano haya kukuza na kuendeleza vipaji vya vijana wetu Jijini Dodoma ili pia wapate fursa ya kuonekana katika maeneneo mbalimbali.”Alisema Mavunde
Alisema  kwa sasa amejipanga kufanya mashindano ya mpira wa miguu kwa kata zote 41 ili kuinua na kuendeleza michezo Jijini Dodoma.
Naye Diwani wa Kata ya Iyumbu, Elias Sutuchi  alisema mashindano yaliyoandaliwa yalikuwa na lengo la kuwahamasisha vijana kuhusu michezo na kuendeleza vipaji kwenye kata, pia amemshukuru Mbunge Mavunde kwa kusaidia kufanikisha fainali hizo.
Mashindano hayo yalishuhudia timu ya Garden FC ya Iyumbu ikiibuka bingwa dhidi ya Ngh’ungugu ya Ihumwa.

Habari Zifananazo

Back to top button