Naibu spika apokea viti vya wagonjwa 20

NAIBU Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu ameshauri zinunuliwe mashine za bei nafuu zinazopima vipimo mbalimbali hospitalini ili kupunguza gharama kubwa kwa wagonjwa wanapofuata huduma hizo.

Zungu ambaye ni mbunge wa Jimbo la Ilala jijini Dar es Salaam, ametoa ushauri huo wakati akipokea viti 20 vya kubebea wagonjwa hospitalini katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Amana vilivyotolewa na Taasisi ya Zam Zam Centre ambapo kati ya hivyo viti 10 vimetolewa kwa Hospitali ya Mnazi Mmoja.

“Gharama za hospitalini bado zipo juu sana, ukitazama mitambo iliyopo katika hospitalini imenunuliwa na serikali, umeme unalipwa na serikali, wataalam wanafundishwa na serikali lakini zipo juu kwa sababu ya mashine hizo zinatoka nje ya nchi hivyo zinauzwa kwa bei kubwa.

Advertisement

“Tubadilishe mitambo kwa kuweka ile inayouzwa kwa gharama nafuu ili wagonjwa wetu wanapopima vipimo mbalimbali wapate unafuu,” amesema.

Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Amana, Dk Gilbert Kwesi ameshukuru kwa msaada huo uliotolewa na taasisi hiyo ya Zam Zam kwa kueleza kuwa serikali na wadau mbalimbali wanafanikisha kutatua changamoto zinazokuwepo.

Amesema kutokana na huduma za kibingwa zinazotolewa hospitalini hapo idadi ya wagonjwa imekuwa ikiongezeka hivyo misaada inayotolewa inasaidia kutatua changamoto mbalimbali zilizopo.

“Kutokana na kuboreshwa kwa huduma za kibingwa kwa siku hospitali hii inapokea wagonjwa 500, kwa takwimu za robo mwaka inapokea wagonjwa 45,000. Lakini katika siku za karibuni kwa idadi ya wagonjwa kwa robo mwaka imefikia 55,000,”amesema.

Naye Mwenyekiti wa taasisi hiyo ya ZamZAM, Sheikh Abass Bantulaki amesema taasisi hiyo inalenga kusaidia jamii na huduma za kiroho hivyo wametoa msaada wa viti hivyo 20 kwa hospitali hiyo ya Amana na Mnazi Mmoja.

“Tumeguswa kwa sababu sisi ni miongoni mwa jamii tunapokuja katika hospitali tunajua nini mahitaji ya hospitali zetu. Kwa hiyo tukaona tutoe kile tulichojaliwa,”amesema.