Mashine ya kukaushia muhogo inavyorahisha upatikanaji unga

TEKNOLOJIA ya mashine ya kukaushia muhogo shambani imewarahisishia wauzaji wa unga unaotokana na zao hilo kupata malighafi kwa urahisi na iliyo safi.

Mkulima wa muhogo Chalinze mkoani Pwani, Gozbart Ndyamkama amesema hayo alipozungumza na HabariLeo katika maonesho ya mazao yaliyofanyika katika viwanja vya Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Kilimo cha Kitropiki (IITA), ikiwa ni sehemu ya program ya kongamano kubwa la chakula lililoanza jana mkoani Dar es Salaam.

Amesema teknolojia ya mashine hiyo imetatua changamoto ya wakulima iliyokuwepo ya kuuza shambani mihogo mibichi ilhali soko kubwa ni la mikavu.

“Kwenye kutatua changamoto ya soko la kuuza muhogo unaotakiwa mkavu, baadhi ya kampuni zilitengeneza teknolojia hii ya mashine ambayo ni ndogo lakini inafanya kazi kubwa ikiwa shambani.

“Mashine ina kisu ambacho inachakata muhogo ambao utaanikwa inatumia muda mchache kukauka, inahitaji kiendesha mwendo yaani mota au injini ambayo inazungusha kisu kinachochakata muhogo.

“Kwa mkulima wa kawaida hiyo mashine unaenda nayo shambani. Lita moja na nusu ya mafuta anaweza kuchakata muhogo tani tatu mpaka nne,” amesema.

Amesema kwa mkulima anapaswa kuandaa mihogo kwa kuimenya, kuosha na kuondoa mchanga wote kisha baada ya kuuchakata kwenye mashine kuuhamisha kwenye kichanja ambapo baada ya saa 24 utakuwa umekauka tayari kwa kuuza.

Amesema muhogo uliochakatwa unanunuliwa na wateja kwa ajili ya kutengeneza unga wa ugali, biscuit pamoja na tambi.

Lakini pia alisema wakulima wamekuwa wakitengenenza muhogo kwa ajili ya viwanda kwa kuusafisha bila kuumenya kisha kuuchakata ukiwa na maganda yake na kuuanika kwa ajili ya viwanda vinavyozalisha vyakula vya mifugo.

“Kwa mfano wateja ni viwanda wanaotengeneza vyakula vya sungura, samaki , vyakula vya kuchangamya kwenye mashudu kuwapa ng’ombe, mbuzi na nguruwe,” amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Uchechemuzi na Uratibu wa Rasilimali kutoka IITA, Dk Regina Kapinga amesema maonesho ya utafiti wa mazao mbalimbali yaliyofanyika katika kituo chao ni miongoni ya program ya kongamano hilo kubwa la chakula lilioanza hapa nchini.

Hivyo kupitia maonesho hayo wadau kutoka sehemu mbalimbali ndani nan je ya nchi wamejionea kile kinachofanyika mashambani zikiwemo tafiti mbalimbali zinazofanyika na zinavyotumika kwenye mikono ya wadau.

“Wapo wakulima, wafanyabiashara wanaooka mikate wameonyesa jinsi wanavyotumia mazao yao kuongeza mnyororo wa thamani kutengeneza bidhaa mbalimbali zikiwemo tambi, mkate, biscut na nyinginezo,” amesema.

Amesema utafiti wa muhogo ni zao ambalo kituo hicho kinafanyia utafiti kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI).

mwisho

Habari Zifananazo

4 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button