DAR ES SALAAM: TAASISI ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) leo imepokea mashine ya kisasa ya kutibu watoto wenye tatizo la vichwa vikubwa yenye thamani ya Sh milioni 500 kutoka kwa Taasisi ya CURE International ya nchini Uganda.
Akizungumza wakati wa kupokea mashine hiyo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa MOI, Prof Abel Makubi amesema tatizo la vichwa vikubwa ni kubwa hapa nchini ambapo kila mwaka wanazaliwa watoto 7,500 na wanaofika hospitali 1500.
“Hii ni idadi ndogo zaidi hapa watoto 5,000 wanabaki bila kufika hospitalini jamii inatakiwa kuhakikisha watoto hawa wanafikishwa kupata huduma za afya kuna wataalamu na mashine zipo na hii ni mashine ya pili kutolewa,”amesema.
Amesema mashine hiyo inayotumika kufanyia upasuaji kwa watoto imekuwa na msaada mkubwa kwani wengi wanakuwa hawana uwezo wa kumudu gharama na taasisi hiyo inatoa vifaa na mafunzo kwa wataalamu.
“Hiki ni kifaa cha pili wametoa na wanashiriki katika ukarabati wa baadhi ya majengo na vyumba vya upasuaji chombo hiki ni kidogo lakini kinakazi kubwa na msaada mkubwa kwani itaboresha huduma na ufanyaji kazi wa upasuaji kichwani na kutibu matatizo hayo ya kichwa kikubwa,”ameeleza Prof Makubi.
Amewashukuru kwa msaada huo na kusema kuwa wako tayari kufanya nao kazi kwa ukaribu kwani watoto wenye vichwa vikubwa wako wengi.
Prof Makubi ametoa wito kwa jamii kuwawahisha hospitali watoto wenye tatizo hilo ili wapate matibabu mapema na haraka.
“Sasa watoto wawili wanaweza kufanyiwa kwa wakati mmoja kupunguza msongamano.
Kwa upande wake Meneja Mipango wa Taasisi ya CURE International, Joshua Menya alisema wao wanatibu watoto walio na vichwa vikubwa na leo (jana)wameungana na MOI kwa miaka saba kuwasiadia watoto hao.
“Tunafurahi kushirikiana na hili tunatoa wito kwa wazazi na wataalamu kuwahudumia watoto hawa vizuri kwani ni watu kama wengine na wanahitaji upendo na huduma nzuri.
Naye Mwangalizi wa Watoto hao,Mchungaji Blandina Chande ameshukuru kwa ushirikiano mkubwa kutoka kwa taasisi hiyo kwani wamekuwa msaada mkubwa kwa watoto hao.
“Sisi ni wasaidizi wa kiroho na kimwili watoto hawa ni zawadi kwa bahati mbaya akitokea mtoto mlemavu mama anaathirika, akinababa vijana wanawakimbia wake zao nitoe wito kwa kwa vijana wasione ulemavu kama tatizo na kuwaacha wamama wakihangaika na watoto wao,”amesisitiza.