“Mashirika ya umma yajifunze kwa binafsi”

ARUSHA: MASHIRIKA ya Umma yametakiwa kujifunza kutoka kwa sekta binafsi kuhusu namna bora ya kuendesha taasisi ili kuongeza ufanisi wao.
Rai hiyo imetolewa leo jijini Arusha na Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko wakati wa kufunga kikao kazi cha wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa taasisi za umma.
Amesema hakuna sababu inayozuia taasisi za umma kuweza kujiendesha kwa ufanisi na weledi na hatimaye kupunguza utegemezi kwa serikali, na badala yake kuwa mstari wa mbele katika kuchangia kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.
“Wakuu wa Taasisi za Umma mnapaswa kuziba mianya ya upotevu wa mapato. Fanyeni kazi ya kusimamia mashirika yenu ili mkawe mafundi wa kurekebisha taasisi zenu na kufikiri tofauti huku mkizingatia ubunifu kama zilivyo sekta binafsi.”
Naye Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Nyongo, aliwapa changamoto wenyeviti na wakuu wa taasisi za umma kuhakikisha wanaiwezesha serikali kutekeleza Dira 2050.



