‘Mashirika yasiyo ya kiserikali yasimamiwe’

MAOFISA Maendeleo ya Jamii wa halmashauri zote nchini wametakiwa kutambua na kufuatilia utekelezaji wa mashirika yasiyo ya kiserikali katika maeneo yao, ili kuhakikisha yanachangia maendeleo kulingana na lengo la kuanzishwa kwao.

Rai hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tamisemi, Ramadhan Kailima katika kikao kazi cha maofisa maendeleo ya jamii kutoka katika sekretarieti za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa kilichofanyika jijini hapa.

Sambamba na hilo, Kailima aliwataka maofisa hao kushirikiana na maofisa lishe katika utekelezaji wa afua za lishe zilizopo katika sekretarieti za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa ili kutokomeza udumavu wa watoto na  kuimarisha lishe bora nchini.

Advertisement

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Zainabu Chaula alisema wizara hizo mbili zinapaswa kuendelea kushirikiana kwa pamoja katika kutoa mafunzo ya kimkakati kwa maofisa maendeleo jamii nchini yenye lengo la kukumbushana mambo mbalimbali ya kiutendaji.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Mwantumu Mahiza aliwataka maofisa hao kuhakikisha wanashirikiana na maofisa elimu katika kutokomeza ukatili wa kijinsia pamoja na mimba za utotoni kwa kuandaa vikao shuleni ili kuleta uelewa na kuvunja ukimya wa ukatili wa kijinsia na mimba za utotoni.