Mashirika yatakayofutwa hadharani mwezi ujao

MSAJILI wa Hazina, Nehemia Mchechu amesema mwezi ujao wanatarajia kutangaza mashirika na kampuni zitakazofutwa, kuunganishwa na zitakazopewa muda wa kurekebisha utendaji kazi wao.

Mchechu alisema hayo Dar es Salaam jana wakati anapokea gawio la Sh bilioni 2.5 kutoka kwa Kampuni ya Kimataifa Kuhifadhi Mafuta ya Petroli Tanzania (TIPER).

Alisema kupitia Ofisi ya Hazina, serikali inataka uwajibikaji na ufanisi katika taasisi zilizo chini yake.

Advertisement

Mchechu alisema kwa sasa ofisi yake inamalizia tathmini kwa mashirika na taasisi zake ili kukamilisha maboresho ambayo Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza yafanyike kuongeza ufanisi.

“Mwezi ujao tutakuwa na kikao na Rais Samia na viongozi wa mashirika na kampuni zenye ubia na serikali, tutatangaza tutakazoziunganisha, kufuta na tutakazozipa muda wa kujirekebisha na baada ya hapo tutaingia kazini,” alisema.

Mchechu alisema katika mabadiliko yatawagusa wakurugenzi wa taasisi husika, wenyeviti na wajumbe wa bodi ambao sasa watalazimika kuwa na ujuzi wa chombo wanachokiongoza.

Mchechu alifafanua kuwa kwa muda mrefu kampuni na mashirika ya umma hayafanyi vizuri kutokana na kutokuwa na viongozi imara hivyo wamedhamiria kufanya mageuzi kurejesha uwajibikaji.

Alisema watasaini mikataba ya ufanisi na wakurugenzi na wenyeviti wa bodi kwa kuwa wanataka watimize walichokubaliana na watakaoshindwa wataondolewa.

Mchechu alisema muda kuwa na maofisa watendaji wakuu na wenyeviti wasio na utaalamu wa eneo wanaloliongoza umepita hivyo hawawezi kuendelea kuwalipa mishahara wenye kuzalisha lakini hawafanyi hivyo.

Alisema kuanzia mwakani watakuwa wanatangaza hadharani mashirika na kampuni zisizofanya vizuri ili zijirekebishe na zikishindwa serikali itachukua hatua zaidi.

Katika kuhakikisha maboresho hayo, Mchechu alisema serikali itayapa mashirika mitaji na kuondoa mifumo yote ya kisiasa inayoingilia na kukwamisha utendaji wao.

Aidha, alisema watafanya marekebisho kwenye sheria na kanuni zinazokwamisha shughuli za mashirika ya umma ili Tanzania ipige hatua zaidi.

“Ukweli tumedhamiria kuongeza mapato na ufanisi, tunataka mashirika na kampuni tunazomiliki asilimia 100 na zile tulizoingia ubia na wenzetu zituletee faida kama ilivyofanya Tiper ambapo tumepata gawio la shilingi bilioni 2.5 kwa mwaka 2022,” alisema.

Aliongeza: “Hatuwezi kutaka ufanisi kwa kuendelea na utaratibu ule ule wa zamani, tutabanana kweli kweli kwenye utendaji kama wanavyofanya katika sekta binafsi.”

Mkurugenzi wa kampuni ya Tiper, Mohamed Mohamed alisema katika kipindi cha miaka 10 wameboresha utendaji kazi na kuwekeza zaidi ya Sh bilioni 73.

Mohamed alisema hivi sasa wana uwezo wa kuhifadhi lita milioni 254 za mafuta kwa mwezi na mpaka mwishoni mwa mwaka huu watakuwa na uwezo wa kupokea lita milioni 314 kwa kuwa wanatarajia kukamilisha miundombinu ya kuweka lita milioni 60.

“Sisi tunaweza kupakua meli ya mafuta kwa siku tatu hadi nne wakati wengine wanafanya kazi hiyo kwa siku nane hadi 10, wanaotumia kampuni yetu wanapunguza gharama kwa asilimia 50 kulinganisha na kwingine,” alisema.

 

3 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *