Mashujaa waurejesha uongozi kunusuru isishuke daraja

Jitihada mbalimbali kufanyika kuhakikisha ina salia Ligi Kuu

KIGOMA: KLABU ya mpira wa miguu, Mashujaa ya mkoani Kigoma imetangaza  utekelezaji wa mipango mbalimbali ya kuinusuru timu hiyo kushuka daraja ikiwemo kuuondoa uongozi uliokabidhiwa timu baada ya timu kupanda Ligi Kuu Tanzania Bara na kuurejesha uongozi uliohangaika na timu hiyo kuipandisha daraja.

Mwenyekiti wa timu ya Mashujaa, Meja Abdul Tika ambaye amerudishwa tena kuiongoza timu hiyo ametangaza hayo kwenye mkutano wa pamoja uliofanyika kwenye Viwanja vya Mwanga Community Centre mjini Kigoma, baina ya uongozi wa timu ukiongozwa na Meja Tika, Kamati ya Hamasa ya Mkoa ikiongoza na Omari Singso na wapenzi wa soka wa mkoa huo.

Mkutano huo unafuatia matokeo mabaya ya timu hiyo ya Mashujaa ambayo imepoteza michezo saba mfululizo huku kukiwa na sintofahamu baina ya uongozi wa timu na mashabiki wa timu hiyo kwa kile kilichoonekana uongozi wa Jeshi kutotaka kuingiliwa kwenye majukumu ya kusimamia timu.

 

Wakizungumza kwenye mkutano huo wapenzi wa soka mkoani Kigoma wamesema kuwa wameshangazwa kuona uongozi wa Jeshi unaondoa viongozi waliopandisha timu, kuondoa idadi kubwa ya wachezaji na kutoshirikisha wananchi kwenye mipango mbalimbali ya kutafutia timu ushindi.

Mmoja wa wapenzi waliohudhuria mkutano huo, Salehe Nassoro amesema kuwa baada ya timu kupanda ligi kuu uongozi wa jeshi ulishindwa kufanya usajili wa maana na hivyo kuleta wachezaji wa kiwango cha chini ambao wameshindwa kuonyesha uwezo wao na kuifanya timu kufika hapo ilipo.

Naye, Hanzuruni Kibera alisema kuwa licha ya wachezaji kuwa na viwango vidogo vya kuweza kushindana wengi hawakuwa na nidhamu na walikuwa wakionekana kwenye mabaa wakizurula hovyo hadi siku ya mechi.

Akijibu mawazo ya mashabiki waliotoa kwenye mkutano huo Mwenyekiti wa timu ya Mashujaa Meja Abdul Tika amesema kuwa baada ya timu kufanya vibaya na wapenzi kuisusa ikiwemo kutohudhuria mechi za timu hiyo kwenye uwanja wa Lake Tanganyika uongozi wa jeshi umekubaliana kwa kauli moja kutafuta suluhu ya kuinusuru timu ikiwemo kuwarudisha wapenzi wa soka mkoani humo kuwa karibu na timu.

Sambamba na hilo Meja Tika alisema kuwa timu imewatimua idadi kubwa ya wachezaji wake kutokana na viwango duni, utovu wa nidhamu na tuhuma za usaliti (kuuza mechi) mambo ambayo yamesababisha timu kupoteza mwelekeo na kukaribia kushuka daraja.

Kutokana na hilo alisema kuwa wameshaanza kufanya usajili wa wachezaji ambapo wachezaji watatu wameshatangazwa akiwemo Balama Mapinduzi (kipenseli), Ramadhani Mtumbuka na Mshambuliaji mmoja wa pembeni aliyefahamika kwa jina la Juma kutoka Inter Star ya Burundi.

Aidha  Pamoja na kurudishwa kwenye uongozi akiwa Mwenyekiti akichukua nafasi ya Meja Mgaya ambaye amepangiwa majukumu mengine amesema kuwa uongozi wa jeshi umemuondoa kwenye nafasi yake Afisa Habari wa timu hiyo, Hamisi Miliango na nafasi hiyo itajazwa na mtu mwingine hivi karibuni akielezwa kuwa miongoni mwa viongozi waliozua taharuki baina ya uongozi wa timu na kamati ya hamasa na wananchi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya hamasa, Omari Singso alisema kuwa waliitwa na uongozi wa makao makuu ya jeshi na kuombwa kurudisha hamasa ya wananchi iliyokuwepo wakati wa kuoandisha timu zikiwa ni salamu kutoka kwa Mkuu wa Majeshi msafara ulioongozwa na Meja Jenerali Mbona

Singso alisema kuwa wamepokea maombi hayo ya Mkuu wa Majeshi na kukubaliana kwa kauli moja kuibeba timu hiyo na ndiyo sababu ya kufanya mkutano huo ili wananchi na wapenzi wote watoe maoni yao ya nini kifanyike kunusuru timu.

Habari Zifananazo

Back to top button