Maswa washangilia ujenzi wa majosho 22

WAFUGAJI katika Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu  wamenufaika na ujenzi wa majosho 22 yaliyojengwa  na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mwaka 2021/2022.

Hayo yameelezwa jana  na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Simon Berege wakati akisoma taarifa kwa Wajumbe wa Kamati ya Fedha , Mipango na Utawala ya halmashauri hiyo katika wa uzinduzi  wa josho jipya la Kijiji cha Dodoma wilayani humo.

Alisema ujenzi huo wa majosho umetekelezwa kwa ushirikiano kati ya serikali kuu, wananchi  na halmashauri ya wilaya hiyo.

Alisema kila josho  limegharimu Sh 19,447,074 kwa mchanganua fedha toka serikali kuu Sh 17,687,074 na nguvu za wananchi Sh 1,760,000 na hadi sasa majosho 20  yamekamilika na yako tayari kwa matumizi huku mawili yakiendelea na ujenzi.

Naye  Kaimu Mkuu wa Idara ya Mifugo katika halmashauri hiyo, Dk James Kawamalwa alisema lengo la serikali kwa ujenzi huo  ni kutokomeza magonjwa yatokanayo na kupe kupitia uogeshaji wa mifugo na kuhakikisha huduma za mifugo zinasogezwa karibu na wafugaji.

Nao baadhi ya wafugaji waliishukuru serikali kwa jitihada wanazozifanya za kuhakikisha wakulima hawapati shida katika mifugo yao.

Kwandu Seni mfugaji wilayani Maswa alisema kupitia majosho hayo wanaamini magonjwa ya kupe yataondoka na mifugo yao itakuwa safi na salama.

Naye Maduhu Ndulu mfugaji wa Kijiji cha Dodoma aliipongeza serikali kwa kutambua umuhimu wa uwepo wa majosho na kupitia majosho hayo yataweza kutokomeza magonjwa yatokanayo na kupe kwani mifugo mingi itakuwa inapata fursa ya kuogeshwa.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button