MAT wazungumzia bima ya afya kwa wote

CHAMA cha Madaktari Tanzania (MAT), kimesema mchakato wa bima ya afya kwa wote ni kuunga mkono mapendekezo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) na kusema kuwa wanaunga mkono asilimia 100 mchakato wake.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Rais wa MAT Dk Deusdedit Ndilanha, pia alitoa mapendekezo ambayo yanatakiwa kuzingatiwa na serikali.

Ndilanha amesema muswada wa bima ya afya kwa wote ni mzuri kwa sababu utakuwa na chombo cha kuratibu na kusimamia mfuko huo  na yale majukumu ya NHIF kuwa  kama  polisi, mahakama wamepunguziwa na wao wanajua mzigo wao ulikuwa mkubwa.

“Jambo lingine tunaloona ya kuwa muswada huu ni muhimu ni hatua tuliyochukua ni muhimu sana kwa mujibu wa WHO, ukitaka kuimarisha huduma za afya unatakiwa kuwa na mambo sita na nguzo kuu ni kugharamia huduma za afya na hizo zingine zinakuwa zimeimarika, tunaona serikali sasa inatekeleza kwa vitendo mapendekezo ya WHO,” ameeleza.

Ndilanha amesema lingine ni uzoefu ambao wameupata kama watoa huduma,  ikilinganisha mapato kabla ya bima ya afya na baada ya bima ya afya utofauti umeonekana  kwamba wameweza kujiendesha kwa watu wachache waliojiunga wameleta mapinduzi, ambapo asilimia 15 ikitolewa na kwenda  kwenye 50 huduma zitaboreshwa zaidi.

Amesema kupitia bima ya afya watakuwa wananchi wameondokana na umasikini kutokana na gharama kubwa za matibabu.

“Fikiria unaambiwa unatatizo la figo na inahitaji kusafishwa mara mbili kwa wiki halafu unaenda kuuza ardhi, nyumba na vyombo naona bima itasaidia sana,”amesisitiza Dk Ndilanha.

Pamoja na hayo amesema endapo watu watakuwa na bima ari ya kutafuta huduma za afya itaongezeka, kwani watakuwa wepesi kwenda hospitali, hivyo ni muhimu serikali kuja na mpango mkakati kwa kutenga fungu maalum litakalosaidia huduma za afya.

Amebainisha kuwa ni muhimu serikali kuja na mpango wa kuhakikisha mfuko huo unakuwa endelevu kwa kuangali namna ya kupata fedha .

Ameiasa serikali kuangalia kwa jicho la tatu ongezeko la watu, kwani linaendana na ongezeko la huduma, hivyo vituo vya afya na wahudumu watatakiwa kuongezeka.

Ametoa rai kwa vituo binafsi na watu binafsi kutumia fursa hiyo kibiashara, kwani watu wengi watatafuta huduma hivyo wawekeze pia itachangia kuondoa tatizo la ajira.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button