JUMLA ya kampuni 34 kutoka Misri zimeshiriki Mkutano wa Kibiashara jijini Dar es Salaam kwa lengo la kutafuta fursa za uwekezaji na biashara zilizopo nchini.
Akizungumza katika mkutano huo ‘B TO B’ ulioandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Balozi wa Misri nchini , Mohamed Abulwafa aliwaeleza washiriki kuwa kampuni zimekuja kujadili na kuona namna ya kuwekeza katika sekta mbalimbali hapa nchini.
“Kikao hiki cha kibiashara kimewakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na Misri kujadili namna kuwekeza katika sekta za dawa, thamani na mbolea…Tanzania ni sehemu sahihi pia bidhaa zetu ni za viwango vya juu na kimataifa hivyo Tanzania itanufaika kutokana na hizi bidhaa,” Mwanadiplomasia huyo ameeleza.,
Balozi huyo aliipongeza Tanzania na kusema kampuni zinatarajia kufungua ofisi zao hapa nchini ikiwa mipango yao itafanikiwa.
“Iwapo mipango yetu itaenda kama tulivyopanga awali, basi, tutafungua ofisi nyingine hapa Tanzania na kuanza kuzalisha hizo bidhaa hapa nchini badala ya kuzisafirisha…tunaishukuru Tanzania na Rais Samia Suluhu kwa kuruhusu uwekezaji wa kampuni mbalimbali hasa sekta ya usafiri wa anga kutokana na uwekezaji huo,” amesema.
Naye Mkurugenzi wa Tantrade’, Latifa Khamisi ametoa wito kwa wafanyabiashara kutumia fursa hiyo ipasavyokujadiliana na kujifunza kutoka kwa wenzao wa Misri.
“Huu ni mkutano muhimu sana kwa Watanzania na upande wa wenzetu Misri…lengo tunaangalia fursa na jambo gani unahitaji tumeshudi. Kuna mikutano mingi ya kibiashara kwa lengo la kuonesha sisi Watanzania tunatakiwa wafanya biashara wetu wajifunze kufanya kujadiliana na wadau wa sekta mbalimbali na uthubutu wa kuingia katika biashara hizo,” ameeleza.
Mkurugenzi wa huduma za wanachama Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Zacky Mbenna amesema taifa la Misri liko mbele kiteknolojia hivyo akawataka wafanyabiashara wa hapa nchini kutumia vema fursa hiyo kujiletea manufaa.
Tangu alipoingia madarakani, Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisitiza juu ya mazingira mazuri ya kufanya biashara.
Wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mawakili wa Serikali katikati ya wiki, Rais aliwataka wadau hao wa sheria kuwa mstari wa mbele kuwasaidia wawekezaji kupitia taaluma zao ikiwepo mashauri yanayowakabili.