UNAPOYATAJA mabadiliko makubwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa huwezi kuacha kuuzungumzia mchango wa familia ya kibiashara ya Salim Abri Asas ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, anasema Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Alfred Mwakalebela.
Dk Mwakalebela anasema Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa iliyopo mjini Iringa inapiga hatua mbalimbali katika kutoa huduma kwa jamii.
Hospitali hiyo imepitia hatua mbalimbali tangu kuanzishwa kwake kabla ya kufikia hatua hiyo ya sasa ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ikiwa na vitanda vya kulaza wagonjwa 600 huku ikipokea wastani wa wagonjwa wa nje 300 na 500 na kulaza kati ya wagonjwa 20 na 60 kwa siku.
Katika mipango yake ya kuboresha huduma, anasema Wizara ya Afya, ina utaratibu wa kuzishindanisha hospitali zake, hususani za rufaa katika maeneo makubwa mawili; kwanza inaangalia namna zinavyotoa huduma kwa wateja wake na pili yanatazamwa mabadiliko makubwa yanayofanywa na hospitali hizo kwa kutumia mapato yake ya ndani.
Katika eneo la utoaji huduma nchini, Dk Mwakalebela anasema mwaka 2022 hospitali yake imeshika nafasi ya nne huku ikipata tuzo baada ya kuwa mshindi wa tatu kwa mabadiliko makubwa inayofanya.
Katika eneo la mabadiliko makubwa, anasema Wizara ya Afya inaangalia jinsi hospitali hizo zinavyotumia mapato yake ya ndani katika kuboresha miundombinu ya kutolea huduma inayohusisha majengo, vifaa, vyoo na njia za kupitishia wagonjwa.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Iringa, Dk Alfred Mwakalebela
Mengine ni pamoja na mapato hayo yanavyotumika katika ununuzi wa dawa na vifaa tiba, motisha kwa wafanyakazi, mafunzo na likizo.
“Kama Wizara ingekuwa inatazama na mchango wa wadau katika eneo la mabadiliko makubwa hususani katika kuboresha miundombinu na upatikaji wa dawa na vifaa tiba, nina hakika kwa mchango mkubwa uliofanywa na mdau wetu Salim Asas hospitali hii ingeshika nafasi ya kwanza,” anasema.
Akiuzungumzia mchango wa Asas katika maboresho ya hospitali hiyo, Dk Mwakalebela anataja mambo makubwa matano yaliyofanywa na mdau huyo wa maendeleo katika eneo la miundombinu ya kutolea huduma za afya kuanzia majengo, upatikanaji wa dawa na vifaa tiba.
“Asas amejenga jengo la kisasa la wagonjwa mahututi (ICU) lenye vitanda nane ambalo baada ya kujengwa lilihifanya hospitali yetu iwe ya kwanza kwa kuwa na ICU bora ikilinganishwa na za hospitali za rufaa za mikoa mingine,” anasema.
Mkurugenzi Mkuu wa Asas Group of Companies Ltd na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Salim Asas
Anasema mchango wa pili uliojengwa na Asas katika hospitali hiyo ni wodi ya kisasa ya watoto wachanga yenye vitanda 60 ambayo ndani yake kuna sehemu ya kulaza watoto njiti na mama zao, na ina hosteli ya mama wanaonyonyesha.
Mchango wa tatu kwa mujibu wa Dk Mwakalebela ni jengo la kituo cha damu salama na vifaa vyake ambalo baada ya kujengwa lilihitofautisha hospitali hiyo na nyingine nyingi ambazo kwa wakati huo zilikuwa zikitumia makontena kwa ajili ya huduma hiyo.
Mchango wa nne uliojengwa na Asas ni jengo la karakana ya viungo bandia pamoja na vifaa vyake vyote uliowezesha majeruhi wa ajali waliokuwa wanalazimika kufuata huduma ya viungo bandia katika mikoa mingine, kuipata ndani ya hospitali hiyo.
Anautaja mchango wa tano kuwa ni wodi maalumu ya kisasa (VIP) iliyojengwa kwa zaidi ya Sh Milioni 600 ambayo ndani yake kuna chumba maalumu (executive room) kwa ajili ya viongozi wa kitaifa wa hadhi ya juu kabisa.
“Tumejenga jengo hilo tukizingatia kwamba kuna viongozi wanakuja mara kwa mara mkoani kwetu kikazi. Hatuombei mabaya lakini tukajiuliza hivi ikitokea viongozi hao wanapata dharula ya ugonjwa wakiwa hapa watapelekwa wapi, ndipo tukaamua kuijenga wodi hiyo,” anasema Asas akielezea kwa kifupi mchango wa familia yake katika maendeleo ya hospitali hiyo.
Asas anasema wamefanya yote haya na watafanya mengine mengi wakiwa kama wadau wa maendeleo ya mkoa wa Iringa ambao wao ni sehemu ya wakazi wake lakini pia kwa kuzingatia kwamba kwa nafasi yao wana wajibu wa kusikiliza mahitaji ya jamii, kushirikiana nao katika miradi ya afya, na kuwezesha ushirikiano wa karibu kati ya hospitali na jamii inayozunguka.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Watoto Dk Tatu Seif
“Wadau tunaweza kutoa mchango ili kuharakisha huduma, hii inaweza kufanyika kwa kusaidia kuboresha miundombinu au kugharamia miradi maalumu ya afya,” anasema.
Mbali na michango mingine iliyofanywa na Asas kuakisi mabadiliko makubwa katika hospitali hiyo, Dk Mwakalebela ameizungumzia wodi ya VIP akisema kwa jinsi ilivyojengwa, vifaa na samani ilizonazo hana uhakika kama kuna wodi inayofanana na hiyo katika hospitali nyingi nchini.
“Tunatamani sana Wizara ya Afya iangalie namna ya kurekebisha taratibu za kuwapata washindi katika maeneo hayo ili kuifanya michango ya wadau iwe sehemu ya mabadiliko, hii itawapa motisha zaidi wadau wetu na kuendelea kuchangia mabadiliko tunayoyazungumza,” anasema.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharula, Dk Huruma Mwasipu
Anasema wakati hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa ikishika nafasi ya tatu, nafasi ya kwanza ilikwenda kwa hospitali ya Maweni ya mkoani Kigoma na ya pili ilichukuliwa na Arusha.
Dk Mwakalebela anasema ubora wa miundombinu ya kutolea huduma ni muhimu sana katika sekta ya afya na huduma za kijamii kwa ujumla kwani huongeza ufanisi wa matibabu, usalama wa wagonjwa na wafanyakazi, upatikanaji wa vifaa tiba na dawa, ubora wa huduma kwa wagonjwa, ufanisi wa utawala na usimamizi na huvutia wataalamu wa afya.
Kuhusu upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika hospitali hiyo, Dk Mwakalebela anamshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipa kipaumbele Sekta ya Afya kwa kutoa rasilimali fedha ili kuimarishaji utoaji wa huduma bora za afya ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya afya.
“Serikali kwa kushirikiana na wadau inaendelea kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na kuimarisha huduma za matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi,”anasema.
Anasema deni walilonalo kwa Rais na watanzania kwa ujumla ni kutoa huduma bora za afya kwa kuzingatia weledi, maadili na miiko ya kitaaluma ya watoa huduma za afya sambamba na kuzingatia utoaji wa huduma nzuri kwa mteja, na matumizi ya lugha ya staha na ya faraja kwa wateja.
Anataja baadhi ya huduma ambazo zilikuwa hazitolewa katika hospitali lakini sasa zinatolewa kuwa ni pamoja na huduma za CT Scan ambayo ni aina ya uchunguzi wa picha za mwili unaozingatia mionzi.
Anasema njia hiyo inaruhusu kupata picha za kina za sehemu mbalimbali za mwili na ni muhimu sana kwa madaktari kufanya utambuzi wa magonjwa, na muundo na hali ya viungo, mishipa ya damu na tishu zingine za mwili.
“Zamani wateja wetu walikuwa wanalazimika kuifuata huduma hii katika hospitali za rufaa Mbeya, Dodomaau Dar es Salaam na hivyo kuwaongezea gharama kubwa za matibabu,” anasema.
Anazitaja huduma zingine zinazotolewa hospitalini hapo ambazo kabla ya mabadiliko yanayoendelea hazikuwepo kuwa ni pamoja na huduma ya X-Ray ya kidigitali, kituo cha kuchuja figo na huduma ya viungo bandia.
Dk Mwakalebela anazungumzia idadi ya wagonjwa katika hospitali hiyo akisema inaelemewa zaidi na watoto na akina mama ambao kwa kuzingatia matatizo yao wanalazimika kutumia rasilimali nyingi kuwahudumia, wakifuatiwa na wagonjwa wa upasuaji.
“Hatuwezi kuwaambia wanawake wasipate ujauzito lakini ombi letu kwao ni vizuri wakapata ushauri kabla ya kuamua kupata ujauzito ili wasijifungue watoto wenye matatizo mengi au wajitahidi wawahi hospitalini mara ya kuwa wajawazito,” anasema.
Daktari bingwa wa magonjwa ya watoto, Dk Tatu Seif anasema mabadiliko yaliyofanywa katika hospitali hiyo yamewatengenezea mazingira mazuri ya kuwahudumia wateja wao.
“Nina mwaka wa 10 katika hospitali hii nikiwa daktari wa kawaida wa watoto na sasa ni daktari bingwa, nikilinganisha mazingira ya utoaji wa huduma huko nyuma na sasa tofauti ni kubwa sana,” anasema.
Anasema wigo wa kutoa huduma za kibingwa katika hospitali hiyo umeongezeka baada ya maboresho yaliyofanywa kwa kutumia rasilimali za serikali, wadau na Asas ambaye mchango wake unaonekana kila mahali katika kuboresha huduma zao.
“Katika kitengo hiki cha watoto, tupo madakatari watatu na tuna kliniki za kibingwa tunafanya kila Jumanne na Alhamis kwahiyo wateja wetu wameokoa gharama za kwenda nje ya Iringa kufuata huduma hizo,” anasema Dk Tatu.
Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharula, Dk
Dk Huruma Mwasipu ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharula hospitalini hapo anasema; “Zamani tulikuwa tunatumia jengo la wagonjwa wa nje (OPD) kutoa huduma za dharula lakini sasa hivi tuna jengo kubwa lenye vifaa vya kisasa.”
“Tulikuwa tunatibu lakini sio kwa ufanisi; na hatukuwa na vifaa vya kisasa kuhudumia majeruhi, na wagonjwa wa moyo, figo, upumuaji na magonjwa mengine waliokuwa wanahitaji huduma za haraka za dharula,” anasema.
Baadhi ya wagonjwa wanaopata huduma katika hospitali hiyo wamekiri kufurahishwa na huduma zinazotolewa ambayo ni ishara nzuri ya ubora wa huduma.
“Tunaridhika na mambo kadhaa ya huduma za afya tunazopata katika hospitali hii ikiwa ni pamoja na upendo na heshima toka kwa watoa huduma, mawasiliano mazuri, ufanisi wa huduma, upatikanaji wa vifaa, mazingira safi na salama na usikivu wa wafanyakazi,” anasema Manase Kaoneka.
Naye Aden Kikoti aliyepata ajali ya bodaboda hivikaribuni na kupatiwa matibabu ya kuwekewa mguu bandia anasema; “Sielewi kama Asas asingejenga karakana hii ingenigharimu kiasi gani kufuata huduma hiyo Dar es Salaam au Dodoma.”
Anasema wafanyakazi wa huduma ya karakana ya kubadilisha viungo bandia wanatoa huduma yenye furaha na kuridhika, jambo linalotoa tafsiri kwamba ni watu wanaojali na wenye uelewa mzuri wa kazi yao.
Naye Farida Kitosi amempongeza Asas akisema kwa kujenga wodi ya watoto yenye huduma mbalimbali ameifanya hospitali hiyo izingatie mahitaji maalumu ya watoto ambayo ni pamoja na mazingira salama, rafiki na yanayoweka kipaumbele ustawi wa watoto.
“Wodi ina mazingira yanayofaa kwa watoto, wafanyakazi waliobobea katika huduma za watoto na matumizi ya teknolojia ya kisasa kutibu watoto,” anasema Kitosi.