Mateja kusakwa kila kona

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imetangaza operesheni maalum nchi nzima kwenye vijiwe vya watumiaji dawa za kulevya maarufu ‘Mateja’ maduka ya dawa na kumbi za starehe zinazoendesha biashara ya Shisha.

Kamishna Jenerali wa DCEA Aretas Lyimo akizungumza leo Januari 25, 2024 amesema operesheni hiyo kali itafanyika nchi kavu na baharini.

Amesema baada ya operesheni kali mkoani Arusha mwaka 2023, wamebaini Mkoa wa Mara na Morogoro kwa sasa inalima bangi kwa wingi wakati mikoa ya Kilimanjaro na Tanga inalima Mirungi kwa wingi.

Advertisement

Amesema, operesheni hizo nchi kavu zitahusisha mashamba ya dawa za kulevya, kwenye mipaka, maeneo ya mijini kwenye vijiwe vya usambazaji na watumiaji wa dawa za kulevya.

Pia kwenye baa na kumbi mbali mbali za starehe ambazo zinajihusisha na biashara ya Shisha ili kubaini matumizi ya dawa za kulevya ambapo wale wote watakaobainika kutumia dawa za kulevya kupitia shisha watachukuliwa hatua kali za kisheria.

“Vile vile operesheni hii itahusisha wauzaji wanaoukiuka taratibu za uuzaji wa dawa tiba zenye asili ya kulevya na kemikali bashirifu,”amesema

Aidha, kwa upande wa baharini, operesheni zitahusisha fukwe na katikati ya bahari.