DODOMA: SERIKALI imesema gharama za usafishaji damu kwa wagonjwa wa figo ‘Dialysis’ inaenda kushuka kwa mwaka wa fedha 2024/2025
Hayo yamesemwa leo Februari 8, 2024 na Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollell akijibu swali na Mbunge wa Kisesa Luhaga Mpina aliyehoji gharama za watu wanaosafisha damu ni kubwa takribani sh 540,000 kwa wiki kwa mwezi Sh milioni 2.1 gharama ambazo wananchi wanashindwa kumudu na kupoteza maisha.
“Sasa haya mambo ya bima, tumejiandaa na bima na nini na bunge hili limeshawahi kutoa misamaha mingi katika maeneo mengi kwa nini sasa wagonjwa wa figo wasitibiwe bure, ukatolewa msamaha na kufidia katika maeneo mengine?” alihoji Mpina
Akijibu swali hilo, Mollel amesema “Wazo la Mbunge ni jema kuna zaidi ya Sh bilioni 70.4 zimesamehewa katika eneo hilo la figo, lakini naomba tutaendelea kuchakata kwa kuwa sasa hivi tunaenda kwenye bajeti na vitu vingine hivyo tunaomba wabunge watupe muda, tunaweza kuhaidi tukashindwa kutekeleza,”amesema Mollel na kuongeza
“Lakini Waziri wa afya ameshafanya kazi kubwa ya kukaa na wataalamu wetu hizi huduma za figo zinaenda kushuka sana kwa sababu tumeshapata namna gani ya kuweza kuzipunguza na tumeshapata watu wanaoweza kutoa dawa na vifaa vinavyotakiwa kwa bei rahisi na huduma hizo zitaenda kushuka sana hazitakuwa kama ilivyo sasa,”amesisitiza Mollel.