Matibabu ya moyo kufanyika mikoani

MKURUGENZI wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam, Dk Peter Kisenge, amesema wana mpango wa kuongeza huduma za matibabu ya moyo katika mikoa mbalimbali nchini, ili kuwafuata wananchi wanaoshindwa kupata huduma.

Dk Kisenge amesema hatua hiyo itaambatana na kwenda kuwafundisha madaktari mikoani, ili waweze kujua jinsi gani ya kuwasaidia wagonjwa wa moyo.

“Malengo yangu ni kudumisha kazi kubwa na nzuri aliyoifanya Prof Janabi (Mkurugenzi aliyepita), taasisi hii imekuwa ikikua kwa kasi, imeng’aa nchini na hata Afrika Masharikia  na Kati,”amesema.

Ameeleza kuwa katika uongozi wake ataongeza vifaa tiba na miundombinu,  ambayo itasaidia madaktari  waweze kufanya upasuaji mkubwa wa moyo wa kisasa zaidi na hata ile ya tundu dogo.

“Niwaeleze wananchi kuwa tutaendelea kudumisha huduma za moyo hapa nchini kwa kuwafanya wananchi kupata  huduma bora zaidi,” ameeleza Dk Kisenge.

Pia amesema kwa  kushirikiana na wizara ya afya wataanzisha mpango wa wananchi  kufanya mazoezi ya kutembea, ili kupunguza  magonjwa ya moyo.

“Wananchi watakuwa wanajiandikisha na tunasema tembea na Jakaya Kikwete, fanya mazoezi ili kulinda moyo, hii ni slogan itazunguka nchi nzima,”amesisitiza Dk Kisenge.

Habari Zifananazo

Back to top button